Kipa Kalambo: Bao la Saido lilikuwa balaa
YANGA imevuna pointi tatu nyingine zilizowafanya wazidi kujikita kileleni, lakini gumzo ni bao tamu la kideoni alililofungwa nyota mpya wa timu hiyo ktoka Burundi, Said Ntibazonkiza ‘Saido’ wakati wakiiangamiza Dodoma Jiji kwa mabao 3-1, huku kipa aliyetunguliwa bao hilo, Aaron Kalambo akishindwa kujiuzuia na kumwagia sifa mfungaji huyo.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha Saido akicheza mechi yake ya kwanza ya ligi akiwa na Yanga alifunga bao la pili kwa friikiki na kuasisti jingine la tatu lililowekwa na beki Bakar Mwamnyeto likitokana pia na friikiki yake.
Akizungumza na Mwanaspoti jana juu ya bao hilo la friikiki ambalo lilimfanya aufuate mpira hewani bila mafanikio na kuipa Yanga bao la pili, kipa kalambo alisema mpigaji alikuwa fundi katika pigo hilo, kwani hakutarajia kama angemtungua namna ile.
Kalambo alisema ingawa anajua ana ubora wa kuzuia mipira ya adhabu, lakini kuna sehemu alizembea katika kufungwa bao hilo la pili katika mchezo huo, huku sehemu kubwa akimsifia Saido akidai alitumia akili na ufundi mkubwa kumuadabisha.
Kipa huyo wa zamani wa Taifa Stars, alisema wakati anaupanga ukuta wake katika adhabu hiyo alijua anayetaka kupiga ni mtu bora katika mipira ya adhabu, hivyo alijipa tahadhari akiupanga vyema ukuta wake, lakini akili nyingi za Saido zilimzidi ujanja.
Kalambo alisisitiza kuwa, Saido alikuwa bora zaidi kushinda akili yake kutokana na jinsi alivyoupinda mpira na kwenda sehemu ambayo hata angenyoosha vipi mkono asingeweza kuzuia usiingie langoni kuipa Yanga bao la pili.
Alisema vipimo vya mpigaji ndio kitu kikubwa anachokisifia katika bao hilo lakini amejifunza kitu kupitia bao hilo na sasa anajipanga kuwa bora zaidi katika mipira ya namna hiyo.
“Kuna taimingi nilikosea katika ule mpira wa adhabu, lakini kubwa nimpe sifa mpigaji nadhani yeye aliweza kutafuta engo na akaupiga mpira kulekule nilipokuwa nimesimama. Unajua katika mipira ya adhabu ni nadra sana kwa mpigaji kupiga kule ambako kipa amesimama,” alisema Kalambo na kuongeza;
“Najua ni makosa kwa kipa kufungwa bao la adhabu sehemu ambayo umesimama, kosa langu lilikuwa ni kuweka hatua moja kutoka ukuta ulipo na hapo ndipo najilaumu sana, ubora wa mpigaji ulikuwa pale aliponiangalia wapio nimesimama na yeye aupige vipi ule mpira.”
“Mpira aliupiga kwa ufundi na akauleta karibu kabisa na mlingoti na ukagonga mwamba na hata nilipojitahidi kutaka kuuzuia, tayari ilikuwa ngumu kifupi niseme acha nimsifie tu mpigaji anajua kufunga kwa mipira ya namna ile,” alisema Kalambo akisisitiza.
KAZE AMSIFIA
Kocha wa Yanga, Cedric Kaze naye alikisifu kiwango cha nyota wake huyo mpya, Saido Ntibazonkiza baada ya kumpa nafasi katika kipindi cha pili akichukua nafasi ya Michael Sarpong, akidai jamaa ni mzuri na ataisaidia sana Yanga kwenye eneo la ufungaji.
Kaze alisema sababu kubwa ya kumpa nafasi ilitokana baada ya washambuliaji wake wengi kupoteza mipira katika kipindi cha kwanza.
“Kulikuwa hakuna utulivu ndio maana nikampa nafasi ya kucheza, ni mchezaji mzuri ambaye aliongeza kitu katika eneo la ushambuliaji na mipira ikawa haipotei. Pia aliongeza utulivu katika eneo hilo na huu ni mwanzo tu naamini huko mbele yatakuja mengi zaidi,” alisema Kaze aliyeiongoza Yanga katika michezo 11 na kushinda nane na mitatu kupata sare.
Mechi tano za awali za Yanga, ilikuwa chini ya Zlatko Krmpotic ambaye alifurushwa ili kumpisha Kaze, lakini naye akishinda michezo minne na kupata sare moja na kuifanya Yanga ikae kileleni kwa sasa ikiwa na pointi 40 kwa michezo 16, ikishinda jumla mechi 12 na sare nne.
IHEFU IJIPANGE
Kocha Kaze pia amesema baada ya kupata pointi tatu katika mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji, akili zake kwa sasa ni kuzikomba nyingine kama hizo kwenye mchezo wao wa keshokutwa dhidi ya Ihefu.
Yanga itavaana na Ihefu jijini Mbeya kwenye mfululizo wa mechi za Ligi Kuu, itakayopigwa Uwanja wa Sokoine, kabla ya kucheza na Singida United baadaye kwa mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la ASFC na kusafiri tena hadi Sumbawanga kuvaana na Prisons katika ligi.
Kaze alisema baada ya mchezo huo akili yake anaigeuzia katika mchezo wao ujao dhidi ya Ihefu kwani anajua ugumu wa wapinzani wao.
“Tunajua Ihefu ni timu nzuri baada ya kuifatilia kwa ukaribu, tunajua namna ya kwenda kupambana na kuchukua pointi tatu muhimu.”
“Mashabiki wajitokeze kwa wingi kwani wanatupa hamasa ya kutosha kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zetu.”
Imeandikwa na
Khatimu Naheka, Dar na Thomas Ng’itu, Arusha