Prime
Kisa Mzize, maskauti Sweden waivamia dabi

Muktasari:
- Msimu huu Mzize amekuwa moto wa kuotea mbali, aliwavutia zaidi maskauti hao alipofunga bao muhimu dhidi ya TP Mazembe katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Mkapa, huku Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1.
MASKAUTI wawili kutoka Sweden, Jamal Osman na Nahom Tesfaye, wameharakisha safari yao kurejea jijini Dar es Salaam ili kuja kumtazama kwa karibu mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize katika mchezo wa watani wa jadi dhidi ya Simba SC, maarufu kama Dabi ya Kariakoo.
Msimu huu Mzize amekuwa moto wa kuotea mbali, aliwavutia zaidi maskauti hao alipofunga bao muhimu dhidi ya TP Mazembe katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Mkapa, huku Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Bao hilo lilionyesha uwezo wake wa kushindana katika kiwango cha juu, jambo lililowashawishi maskauti hao ambao wameletwa na taasisi ya AYE kuongeza umakini katika kumchunguza.
Osman na Tesfaye walikuwa Zanzibar wakisaka vipaji vya wachezaji chipukizi, lakini jina la Mzize limewalazimu kufupisha muda wao visiwani humo na kurejea haraka bara. Wawili hao wamekuwa wakimfuatilia mshambuliaji huyo tangu wakiwa barani Ulaya, na sasa wanataka kumtazama kwa macho yao katika mojawapo ya mechi kubwa zaidi Afrika Mashariki.
Kwa sasa, mshambuliaji huyo mwenye kipaji kikubwa anaongoza katika orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu Bara, akiwa na mabao 10, sawa na Jean Charles Ahoua wa Simba na Prince Dube. Rekodi hiyo imemfanya kuwa mmoja wa wachezaji wanaovutia macho ya maskauti mbalimbali.
Akizungumza kuhusu uwezo wa Mzize, Osman alisema: “Tumevutiwa naye tangu tukiwa Ulaya. Ana kasi nzuri, uwezo mkubwa wa kumalizia mashambulizi, na anaonyesha ukomavu mkubwa licha ya umri wake mdogo. Tumemwona kwenye video, lakini tunahitaji kumuangalia kwa karibu kwenye mechi kubwa kama hii.”
Osman alisisitiza kuwa Dabi ya Kariakoo ni mchezo sahihi wa kumpima mshambuliaji huyo, kwani utakuwa na presha kubwa, mashabiki lukuki, na ushindani mkali. “Mechi za watani wa jadi huwa zinatoa picha halisi ya uwezo wa mchezaji. Ikiwa atang’ara dhidi ya Simba, basi tutakuwa na uhakika zaidi wa kile tunachokiona ndani yake,” aliongeza.
Kwa upande wake, Tesfaye alibainisha kuwa wanasaka mshambuliaji mwenye sifa za kimataifa, na Mzize anaonekana kuwa na vigezo hivyo.
“Soka la Ulaya linahitaji wachezaji wenye maamuzi sahihi, uwezo wa kucheza kwa kasi na nidhamu ya hali ya juu. Tunataka kuona kama Mzize anaweza kucheza kwa kiwango kilekile chini ya presha,” alisema Tesfaye.
Mbali na maskauti wa Sweden, taarifa zinaeleza kuwa pia kuna wawakilishi wa vilabu vingine vya nje watakaokuwepo kushuhudia mchezo huo, wakisaka vipaji vya kuongeza kwenye vikosi vyao. Hii inaonyesha namna soka la Tanzania linavyozidi kuvutia macho ya dunia.
Kwa sasa, mashabiki wa Yanga wanamtegemea Mzize kuonyesha ubora wake na kuwapa furaha ya ushindi katika dabi hii. Swali kubwa ni je, ataweza kuonyesha kiwango chake mbele ya maskauti na kujiwekea nafasi ya kusajiliwa nje ya nchi?
Jibu litapatikana ndani ya dakika 90 za Dabi ya Kariakoo, mchezo ambao utakuwa kipimo kikubwa kwa mshambuliaji huyo chipukizi.