Kocha JKT Tanzania aanika usajili mpya

Muktasari:
- Maafande hao wa JKT wanaokamata nafasi ya sita katika msimamo wakiwa na pointi 35 wakicheza mechi 28, hivi karibuni walitolewa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) na kuikosa tiketi ya CAF kwa michuano ya Kombe la Shirikisho waliyoisotea kwa karibu miaka 23 tangu walipobeba kombe 2002.
KOCHA Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amefichua juu ya mpango wa kuboresha kikosi katika dirisha kubwa la usajili baada ya kushindwa kufikia malengo msimu huu, huku akitaja maeneo mawili atakayoshughulika nayo ili maafande hao warudi na moto katika Ligi Kuu Bara.
Maafande hao wa JKT wanaokamata nafasi ya sita katika msimamo wakiwa na pointi 35 wakicheza mechi 28, hivi karibuni walitolewa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) na kuikosa tiketi ya CAF kwa michuano ya Kombe la Shirikisho waliyoisotea kwa karibu miaka 23 tangu walipobeba kombe 2002.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Ahmad alisema JKT imeshindwa kufikia malengo msimu huu kutokana na kuangushwa na baadhi ya nafasi zilizoshindwa kuonyesha makali hivyo mchakato umeanza kuhakikisha wanafanya usajili kwa kuboresha safu ya ushambuliaji na kiungo.
Maeneo hayo ya kiungo na ushambuliaji yana vichwa kama Hassan Dilunga, Said Ndemla, Ismail Aziz Kader, Maka Edward, Shiza Kichuya, Bakar Mohammed, John Bocco, Matteo Antony, Edward Songo na wengine walioiwezesha timu hiyo kufunga mabao 27 na yenyewe kuruhusu 26 katika mechi 28.

“Mpango wetu ulikuwa ni kumaliza tano bora lakini mambo yameenda tofauti hii ni kutokana na ugumu tuliokutana nao kutoka kwa wapinzani hatupo nafasi mbaa lakini ushindani ni mkubwa, tunapaswa kuwa na kikosi imara chenye wachezaji wenye uwezo na uzoefu ambao watatufikisha kwenye malengo yetu,” alisema Ahmad na kuongeza:
“Usajili bora ndio unakupa mafanikio hicho ndio kilichotokea kwa baadhi ya timu ambazo zimefikia malengo tumeona upungufu tutatumia dirisha lijalo kujiimarisha tayari kwa ushindani msimu ujao.”
Ahmad alisema msimu huu maeneo mawili safu ya ushambuliaji kuanzia kiungo hawakuwa vizuri hivyo kukosa umakini na makali katika upachikaji mabao na kujikuta wakishindwa kuonyesha ushindani.
Alisema anaridhishwa na viwango vya wachezaji waliopo na upambanaji wao, lakini kutokana na ugumu wa ligi msimu huu anahitaji kuwa na kikosi imara ambacho hakitegemei mchezaji mmoja.

Katika mechi 28 ilizocheza JKT Tanzania imefunga jumla ya mabao 27, huku yenyewe ikiruhusu 26, ikishinda mara nane tu, na kupoteza tisa, lakini ikiwa ndio vinara wa kupata sare ikiwa na 11 ikifuatiwa na Wagosi wa Kaya, Coastal Union iliyotoka sare 10, japo yenyewe ina pointi 31 ikiwa nafasi ya 10.
Maafande hao wana mechi mbili zote za ugenini ikianza dhidi ya Pamba Jiji Juni 18 kisha kumaliza msimu na Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma siku ya Juni 22.