Kocha Tabora United ajichomoa

Muktasari:
- Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo, zimeliambia Mwanaspoti kuwa, kocha huyo amejiweka pembeni kutokana na kutoridhishwa na kile kinachoendelea kikosini, hasa kukosa sapoti ya kutosha inayochangia timu kufanya pia vibaya tangu ametua kikosini humo.
KOCHA Mkuu wa Tabora United, Mzimbabwe Genesis ‘Kaka’ Mangombe imedaiwa amejiweka kando kukifundisha kikosi hicho, huku sababu kubwa ikielezwa ni kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo ikiwa ni siku zisizofikia 20 tangu amejiunga nayo Machi 28, 2025.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo, zimeliambia Mwanaspoti kuwa, kocha huyo amejiweka pembeni kutokana na kutoridhishwa na kile kinachoendelea kikosini, hasa kukosa sapoti ya kutosha inayochangia timu kufanya pia vibaya tangu ametua kikosini humo.
“Kuna mambo hayaendi sawa ambayo yamemfanya kujiweka pembeni, suala la mwenendo mbaya ni kweli lipo ila kitendo cha yeye kutopewa stahiki zake ndicho kilimfanya ajisikie vibaya na kuona hathaminiwi ipasavyo,” kilisema chanzo.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tabora United (CEO), Charles Obiny alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, alisema kwa sasa kuna mambo wanayoendelea nayo na yatakapokamilika wataweka wazi, ingawa hawezi kukubali wala kukataa ishu ya kocha.
Kocha huyo aliyezifundisha Dynamos na Yadah Stars zote za Zimbabwe, tangu ajiunge na Tabora Machi 28, mwaka huu, ameiongoza katika michezo minne ambapo mmoja pekee ni wa Kombe la Shirikisho (FA), na mitatu ni ya Ligi Kuu Bara.
Katika michezo hiyo, Mangombe amepoteza yote akianza kwa kutolewa na Kagera Sugar kwa penalti 5-4, baada ya sare ya bao 1-1 ya dakika 90 katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho, huku Ligi Kuu akichapwa na Yanga mabao 3-0, Aprili 2.
Baada ya hapo, Mangombe aliyechukua nafasi ya Mkongomani Anicet Kiazayidi, akachapwa tena bao 1-0, dhidi ya Pamba Jiji Aprili 5, huku mchezo wa mwisho ni wa kichapo kutoka kwa ‘Wazee wa Mapigo na Mwendo’, Mashujaa FC cha 3-0, Aprili 10.
Tabora msimu huu imefundishwa na makocha watatu tofauti ikianza na Mkenya Francis Kimanzi aliyeondoka Oktoba 21, 2024, baada ya kuiongoza katika michezo minane ya Ligi Kuu, na kati ya hiyo alishinda miwili, sare miwili na kupoteza minne.
Kitendo cha kuondoka Kimanzi, uongozi wa Tabora ukamtambulisha, Mkongomani Anicet Kiazayidi ambaye tangu ajiunge na timu hiyo Novemba 2, 2024, aliiongoza katika michezo 14 ya Ligi Kuu, ambapo alishinda saba, sare mitano na kuchapwa miwili.