Kocha: Wazir anastahili kuwamo Stars

Muktasari:

  • Kocha Mkuu wa KMC, Moalin amesema matarajio yake ni kuona Wazir Junior anajumuishwa katika kikosi cha Stars katika uteuzi ujao kutokana kiwango alichonacho hivi sasa.

Mbeya. Wakati baadhi ya wadau na mashabiki wa soka nchini wakihoji kukosekana kwa straika Waziri Junior katika kikosi cha timu ya Taifa ' Taifa Stars' Kocha Mkuu wa KMC, Abdulhamid Moalin amesema ni muda wa nyota huyo kujumuishwa kutokana na kiwango alichonacho hivi sasa.

 Moalin pia amesema kwa mwenendo wa nyota huyo anaamini katika uteuzi ujao wa wachezaji katika timu ya Taifa, straika huyo ataitwa kwani ndiye mchezaji mzawa anayeongoza kwa idadi ya mabao.

Wazir aliyewahi kuitumikia Toto Africans na Mbao FC za jijini Mwanza kabla ya kutimkia Yanga kwa sasa ni mali ya KMC na amekuwa na kiwango bora akiwa ametupia mabao 11 akiachwa mawili na vinara Stephen Aziz Ki (Yanga) na Feisal Salum wa Azam FC.

Pia nyota huyo ndiye straika mzawa anayeongoza kwa mabao akifuatiwa staa wa Peisons,  Samson Mbangula mwenye manane sawa na kiungo wa Yanga, Mudathir Yahya akiwa na winga, Adam Adam wa Mashujaa akiwa nayo saba.

Akizungumza jijini hapa, Moalin amesema anashangaa kuona Wazir anasahaulika ukilinganisha na straika wengine wa Stars kwani hakuna anayemfikia kwa idadi ya mabao kwa wachezaji wa ndani na anastahili kuwamo kikosini.

"Ni straika gani mzawa anayemzidi mabao Wazir? Anastahili kuwamo kikosi cha Stars kutokana na kiwango chake kwa sasa alichonacho na anaweza kufanya vizuri," amesema Moalin.

Kuhusu mbio za ufungaji bora msimu huu, kocha huyo amesema kwa sasa wanaendelea kumpa nafasi nyota huyo na kumtengenezea nafasi inapopatikana aweze kutupia mabao.

Amekiri ushindani kuwa mkali kwa sasa akieleza namna benchi la ufundi linavyoitengeneza timu na mchezaji mmoja mmoja, Wazir anaweza kupenya na kutwaa tuzo ya mfungaji bora msimu huu.

"Kama kocha au benchi la ufundi tunaendelea kumtengeneza na kuiweka vyema timu na mchezaji mwenyewe kumpa nafasi ili aweze kufunga mabao na lolote linawezekana," amesema kocha huyo.