Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ligi Kuu Bara leo ni mechi za kimkakati

Muktasari:

  • Duru la kwanza tumeshuhudia timu zikiwa na hesabu tofauti, nyingi zikionekana kutofanya vizuri ikiwemo KenGold na Pamba Jiji zilizopanda daraja, lakini duru la pili hakuna aliyekuja kinyonge, hata hao wageni wa ligi wameonyesha maajabu.

LIGI Kuu Bara imeanza kuchangamka kwani ngwe ya lala salama imezifanya kila timu iingie uwanjani ikiwa na mkakati mkali sana kulinganisha na ilivyokuwa awali.

Duru la kwanza tumeshuhudia timu zikiwa na hesabu tofauti, nyingi zikionekana kutofanya vizuri ikiwemo KenGold na Pamba Jiji zilizopanda daraja, lakini duru la pili hakuna aliyekuja kinyonge, hata hao wageni wa ligi wameonyesha maajabu.

Mikakati iliyopo kwa kila timu hivi sasa inaifanya ligi hiyo kuzidisha ushindani ambao tunakwenda kuushuhudia leo pale ambapo mechi tatu zitakapochezwa katika miji miwili tofauti.

Mechi hizo za leo zimepangiliwa vizuri sana na kutoa nafasi kwa watazamaji kuifuatilia moja baada ya nyingine kwa utulivu wa hali ya juu, yaani hakuna kushika rimoti kubadili chaneli. Ukianza kutulia kwenye runinga yako kuanzia saa 10 jioni, ni burudani tu ya soka la Kibongo hadi saa 3 usiku.

Kumbuka hii ni raundi ya 23 katika duru la pili ambapo ikimalizika hapa tutabakiwa na raundi saba pekee kuhitimisha msimu Mei 25, 2025 ambapo itafahamika rasmi nani anakwenda Championship, anayebaki na atakayepata nafasi ya kujitetea kwa kucheza play off.


KMC v FOUNTAIN GATE

Ni mchezo wa kwanza kupigwa leo umepangwa kuanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, ambapo wenyeji KMC chini ya kocha Kally Ongala, wana kazi ya kujibu mapigo ya Fountain Gate baada ya duru la kwanza kulala mabao 3-1 ugenini huku ikipata pigo la nyota wake Ibrahim Elias kuonyeshwa kadi nyekundu.

Pengine kadi hiyo nyekundu ya kipindi cha kwanza iliwatibulia mipango KMC na kupokea kichapo hicho kwani kabla ya tukio hilo, walikuwa nyuma kwa mabao 2-0.

Jambo jingine linalovutia katika mchezo huu ni namna timu zinazokwenda kukutana nafasi zao zilivyo katika msimamo.

Kwa sasa KMC inayoshika nafasi ya 10, imezidiwa pointi moja na Fountain iliyopo nafasi ya nane. Hiyo inatoa majibu ya kwamba hakuna ambaye atakubali kuwa mnyonge.

Rekodi zinaonyesha timu zote si nzuri katika kuzuia kwani KMC imeruhusu mabao 32, ikiwa ni timu ya tatu kwa kuruhusu mabao mengi msimu huu, huku Fountain ikiwa ndio vinara wakifungwa 39 kabla ya jana KenGold kucheza dhidi ya Mashujaa kwani ilikuwa timu ya pili kwa kuruhusu mabao mengi (38).

Kitendo cha safu zote za ulinzi za timu hizo kuonekana kuruhusu kirahisi mabao, kinaweza kuifanya mechi hii kuwa ya mabao kama ilivyokuwa duru la kwanza yalipozalishwa mabao manne.

Timu hizi zinakutana duru la pili zikiwa na makocha wapya kwani Ongala alikabidhiwa kuiongoza KMC Novemba 14, 2024 baada ya kuondoka Abdihamid Moallin aliyekuwepo awali walipofungwa 3-1 huku Robert Matano aliyetua Fountain Gate Januari 10, 2025, amechukua nafasi ya Mohamed Muya.

Katika mechi sita za ligi ambazo Matano ameiongoza Fountain Gate, ameshinda moja pekee, huku sare zikiwa mbili na kupoteza tatu, wakati Ongala tangu Novemba 14, 2024, ameiongoza KMC kucheza mechi 11, ameshinda mbili, sare nne na kupoteza tano. Matokeo hayo si mazuri kwa wote. 


NAMUNGO V SINGIDA BS

Saa 1:00 usiku itakuwa zamu ya Namungo kuwakaribisha Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi. Ni mchezo ambao Namungo ina nafasi ya kujiuliza kwani haina rekodi nzuri nyumbani ikiwa ndio timu iliyokusanya pointi chache zaidi (9) kufuatia kushinda mbili, sare tatu na kupoteza tano kati ya mechi 10 zilizopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa.

Tangu Oktoba 28, 2024 Namungo ilipoichapa Pamba Jiji bao 1-0 nyumbani, haijapata ushindi wowote hapo katika mechi tano zilizofuatia, imefungwa mbili dhidi ya Simba na Yanga na kutoka sare tatu, hivyo kocha Juma Mgunda na vijana wake wana mtihani wanaopaswa kukabiliana nao vizuri ili kuondoa rekodi hiyo mbaya.

Singida rekodi zake zinaridhisha kidogo inapokuwa ugenini kwani imekusanya pointi 19 katika mechi 10, inaingia kwenye mchezo huu ikiwa na kumbukumbu bora dhidi ya Namungo baada ya duru la kwanza kuichapa 2-0 pale Uwanja wa Liti mkoani Singida.

Kinachowapa jeuri zaidi Singida BS ni namna safu yake ya ushambuliaji ilivyokuwa moto tangu duru la pili hasa baada ya kufanya maboresho ya kikosi chao kwa kuongeza nyota wanaocheka na nyavu akiwamo Jonathan Sowah.

Sowah aliyejiunga na timu hiyo dirisha dogo lililofungwa Januari 15, 2025, katika mechi sita ambazo timu hiyo imecheza tangu hapo ikifunga mabao tisa, nyota huyo raia wa Ghana amefunga mabao sita peke yake, akiwa na wastani wa kufunga bao moja kila mechi.

Safu ya ulinzi ya Namungo yenye wachezaji wazoefu kama Daniel Amoah na Erasto Nyoni ina kazi ya kufanya kuiokoa timu yao na majanga kwani haipo salama kwenye msimamo ikiwa nafasi ya 12 na pointi zake 23, huku Singida Black Stars ikipambana kutotoka nne bora ikishika nafasi ya nne na pointi 41, ikizidiwa 4 tu na Azam iliyo juu yake.


AZAM V TZ PRISONS

Ni mtihani mwingine kwa kocha Aman Josiah wa Tanzania Prisons ambaye amekabidhiwa majukumu ya kuhakikisha anamaliza salama mechi zilizobaki kwani timu hiyo nafasi yake ya 14 iliyopo na pointi 18, inaiweka kwenye hatari ya kushuka daraja.

Prisons inakwenda kuikabili Azam ugenini kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar kuanzia saa 3 usiku.

Azam nayo imetoka kupata matokeo yasiyoridhisha ambayo ni sare tatu mfululizo dhidi ya Coastal (0-0), Simba (2-2) na Namungo (1-1), lakini pia ina machungu ya kuondoshwa hatua ya 32 bora ya Kombe la FA dhidi ya Mbeya City, hivyo inaweza kuutumia mchezo huu dhidi ya Tanzania Prisons kurejea kwenye hali ya ushindi na kulipa kisasi kwa vijana hao wa Jiji la Mbeya.

Rekodi za mechi za ugenini zinaihukumu Tanzania Prisons inapokwenda kukabiliana na Azam kwani timu hiyo imekusanya pointi nne pekee wakati wenyeji wao wakiwa nyumbani ni moto wakikusanya pointi 26 katika mechi 11.

Katika taswira nyingine, Azam inapambana isishuke zaidi ya nafasi ya tatu iliyopo kwa sasa na pointi zake 45 ili kujihakikishia moja kwa moja kupata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao baada ya kubaki na tumaini pekee la kufanya vizuri kwenye ligi kuipata nafasi hiyo kutokana na kuondoka Kombe la FA ambapo bingwa wake ndiye mwakilishi namba moja wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha wa Azam, Rachid Taoussi raia wa Morocco, anautazamia mchezo huu na mingine iliyobaki kama sehemu ya kurekebisha pale walipokosea ili kumaliza ligi vizuri.

“Tunataka kufanya vizuri mechi zilizobaki, haijalishi nyumbani au ugenini, mahitaji ya timu ni kurejea tena michuano ya kimataifa kwa msimu ujao,” alisema Taoussi ambaye huu ni msimu wake wa kwanza kufundisha Tanzania akitua Azam Septemba 5, 2024 na kuchukua nafasi ya Youssouph Dabo kutoka Senegal.