Prime
Maajabu mawili ubingwa wa Yanga
NDANI ya shangwe la Yanga kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC kwa mara ya 32 tangu mwaka 1965, kuna maajabu mawili ya kuvutia na rekodi nzuri ambayo kikosi hicho imeweka.
Moja ya rekodi ya kuvutia kwa Yanga ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu mara tano mfululizo ikiwa ni mara ya pili kwa timu hiyo kufanya hivyo, ikiwa ni miongoni mwa maajabu na kuwapiga bao watani wao wa jadi, Simba.
Yanga ndio timu ya kwanza kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tano mfululizo kuanzia mwaka 1968, 1969, 1970, 1971 na 1972, kisha Simba ikajibu mapigo na kutwaa taji hilo mara tano mfululizo miaka ya 1976, 1977, 1978, 1979 na 1980.
Baada ya Simba kusawazisha, Yanga ikaandika rekodi nyingine ya kutwaa taji hilo mara tano mfululizo kuanzia msimu wa 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024, 2024-2025 na 2025-2026, ikiwa ni kwa mara ya pili tangu Ligi Kuu Bara ilipoanza mwaka 1965.
Maajabu mengine ya Yanga iliyofanya msimu huu ni ya kushinda ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC huku ikitoka kuchukua Kombe la Mapinduzi 2026, jambo ambalo lilikuwa halijawahi kutokea bingwa wa michuano hiyo akashinda Ligi Kuu Bara tangu mwaka 2007.
Mwaka 2007, Yanga ilichukua ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, japo msimu wa 2006-2007, Simba ilikuwa mabingwa wa Ligi ndogo iliyotumika ili kumpata mshindi wa kupeperusha bendera ya Tanzania kimataifa.
Baada ya hapo, mwaka 2008, Simba ikatwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi, ilivyokuja Bara taji likachukuliwa na Yanga msimu wa 2007-2008, huku 2011, miamba hiyo ikakutana katika fainali na kikosi hicho cha Msimbazi kikashinda mabao 2-1.
Kushinda kwa Simba ubingwa huo wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2011, ikaendeleza nuksi kwani ilikosa ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa 2010-2011 na kushuhudiwa kikosi cha Yanga kikitwaa taji hilo, ikiwa ni mwendelezo wa maajabu ya michuano hiyo.
Mwaka 2021, Yanga ilifika fainali ya Kombe la Mapinduzi na kuichapa Simba kwa penalti 4-3, baada ya suluhu (0-0), ila kikosi hicho chenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani kilivyorudi huku Bara kilikosa ubingwa msimu wa 2020-2021.
Msimu huo wa 2020-2021, ubingwa wa Ligi Kuu Bara ulienda Simba ikiwa ni msimu wa mwisho kwa kikosi hicho kuchukua na wa nne mfululizo kutwaa pia, baada ya awali kufanya hivyo, kuanzia msimu wa 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021.
Fainali ya mwaka 2026, Yanga ilishinda Kombe la Mapinduzi kwa kuifunga Azam kwa penalti 5-4, baada ya suluhu (0-0) dakika 120, Januari 13, 2026, kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba, kisha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ikiwa ni rekodi mpya.
Kushinda kwa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu msimu wa 2025-2026, imeweka rekodi mpya ya timu ya kwanza kutwaa taji hilo huku ikitoka kuchukua pia Kombe la Mapinduzi, tangu michuano hiyo inayofanyika visiwani Zanzibar ilivyoanza mwaka 2007.