Malindi yakubali yaishe Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Timu hiyo iliyocheza mechi 27 hadi sasa ikibakiwa na tatu kumaliza msimu huu, ina pointi 25 ambazo hata ikishinda haiwezi kuondoka kwenye mstari wa kushuka daraja ikiungana na New Stone Town na Junguni.
MENEJA wa timu ya Malindi, Ramadhan Sanga amekubali yaishe kwa timu yake kushuka daraja msimu huu huku akisema wana mikakati madhubuti ya kurejea Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).
Amesema wanakwenda kucheza Ligi Daraja la Kwanza kwa msimu mmoja pekee na kurudi Ligi Kuu kumalizia walipoishia.
Ametoa sababu ya kushuka kwao ni sintofahamu zilizokuwa zinaendelea klabuni hapo kwani ziliifanya timu kuyumba na hatimaye kushindwa kufanya vizuri.
“Migogoro iliyokuwepo ndani ya timu imechangia kwa kiasi kubwa timu kushuka daraja lakini tutarudi Ligi Kuu kwa kishindo,” amesema.
Meneja huyo amesema, Malindi haikupaswa kushuka kwa mechi 10 walizokuwa nazo kwani walikuwa na kila sababu ya kujitetea kuendelea kusalia kwenye ligi hiyo.
Amesema, mipango na mikakati yote wanailekeza kwenye Ligi Daraja la Kwanza kwa lengo la kupindua meza na kucheza tena Ligi Kuu.
Malindi ambayo baada ya mechi sita za kwanza msimu huu ilikuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar ikikusanya pointi 14, ghafla kibao kikageuka kwani mechi 21 zilizofuatia ikakusanya pointi 11 na kufanya jumla kuwa 25 zilizoishusha daraja ikikamata nafasi ya 14.
Timu hiyo iliyocheza mechi 27 hadi sasa ikibakiwa na tatu kumaliza msimu huu, ina pointi 25 ambazo hata ikishinda haiwezi kuondoka kwenye mstari wa kushuka daraja ikiungana na New Stone Town na Junguni.