Maxime asaka dawa ya mabao Dodoma Jiji

Muktasari:
- Dodoma Jiji ipo nafasi ya nane baada ya kucheza mechi 23, ikikusanya pointi 27, imefunga mabao 22 huku ikiruhusu mabao 23 ikiwa na wastani wa kuruhusu bao kila mchezo.
KOCHA Mkuu wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime amesema moja ya kazi anayoendelea kuifanya kwenye uwanja wa mazoezi ni kuinoa zaidi safu yake ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikipoteza nafasi wanazozitengeneza.
Dodoma Jiji ipo nafasi ya nane baada ya kucheza mechi 23, ikikusanya pointi 27, imefunga mabao 22 huku ikiruhusu mabao 23 ikiwa na wastani wa kuruhusu bao kila mchezo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Maxime alisema safu ya ushambuliaji ina changamoto licha ya kutengeneza nafasi inashindwa kuzitumia, hivyo ameamua kulisimamia hilo kwa kumtaka kila mchezaji kutumia nafasi bila kuangalia mshambuliaji.
“Haiwezekani timu ikawa nyuma kwa mabao dhidi ya michezo tuliyocheza, hii sio nzuri kwetu, pointi ni chache, hatupo kwenye nafasi nzuri ukilinganisha na washindani wenzetu, hivyo napambana kuhakikisha napunguza makosa eneo la kushambulia,” alisema na kuongeza.
“Tumepata wakati mzuri wa kucheza mechi mbili za kirafiki kipindi hiki ligi ikiwa imesimama, nimeona mabadiliko maeneo mawili ulinzi na ushambuliaji kwani tumeshinda mchezo mmoja na suluhu moja.”
Dodoma Jiji mechi zote mbili wamecheza dhidi ya Namungo mchezo wa kwanza walimaliza kwa suluhu huku wa pili wakiibuka na ushindi wa mabao 3-0 kitu ambacho Maxime amekiri washambuliaji wake wameanza kufanyia kazi maelekezo yake.
Akizungumzia mchezo ujao wa ligi dhidi ya JKT Tanzania ugenini utakaochezwa Aprili 2 mwaka huu, Maxime alisema hautokuwa rahisi kwa sababu wanaenda kucheza ugenini uwanja ambao wenyeji wanarekodi nzuri nao.