Mbangula atengewa ufalme Prisons

Muktasari:

  • Hadi sasa wachezaji Stephane Aziz Ki (Yanga) na Feisal Salum (Azam), wanaongoza kwa idadi ya mabao 13 kila mmoja, Wazir Junior wa KMC akifuata kwa mabao 11, huku Maxi Nzengeli wa Yanga akiwa nayo tisa.

KOCHA Mkuu wa Tanzania Prisons, Ahmad Ally, ameangalia vita ya ufungaji bora kwenye Ligi Kuu Bara na kumsukia mkakati straika wake, Samson Mbangula kuhakikisha anachomoza kwenye kinyang’anyiro hicho.

Hadi sasa wachezaji Stephane Aziz Ki (Yanga) na Feisal Salum (Azam), wanaongoza kwa idadi ya mabao 13 kila mmoja, Wazir Junior wa KMC akifuata kwa mabao 11, huku Maxi Nzengeli wa Yanga akiwa nayo tisa.

Mbangula anafuata kwenye orodha hiyo katika nafasi ya tano kwa vinara wa mabao akiwa ametupia nane na kuweka upinzani mkali kwenye kuwania Tuzo ya Ufungaji Bora.

Kocha Ally alisema katika kuhakikisha nyota wake anafanya vizuri, anaendelea kumpa nafasi, lakini kumuwekea program maalumu haswa za kufunga mabao ili kuwaacha wapinzani wake.

Ally hakusita kumpongeza staa huyo kutokana na kazi nzuri anayoifanya kuisaidia Prisons kwenye kuipa matokeo mazuri akieleza kuwa benchi la ufundi linamtazama kwa jicho la tatu.

“Anafanya vizuri, lazima sisi benchi la ufundi tumpe kitu kingine cha ziada mazoezini ili kufikia malengo yake, mafanikio yake ni yetu kwa ujumla, ushindani ni mkali,” alisema Ally.

Kocha huyo alisema anaendelea kutengeneza muunganiko wa timu haswa safu ya ushambuliaji baada ya pacha baina ya Mbangula na Zabona Hamis kuonesha matumaini.

Kabla ya ligi kusimama, Mbangula na Zabona walikuwa na maelewano mazuri eneo la ushambuliaji wakihusika kwenye mabao saba na asisti sita kwa pamoja na kuiweka timu hiyo nafasi ya tano kwenye msimamo kwa pointi 28.