Mtibwa wavuliwa ubingwa, Simba na Yanga hawakutani nusu fainali

Mtibwa Sugar jana Jumamosi ilivua rasmi taji lake la Kombe la Mapinduzi baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Simba huku Wekundu hao nao hawataweza kucheza nusu fainali na watani wao Yanga.
Katika mechi hiyo ambayo ilikuwa ni ya mwisho hatua ya makundi, Simba iliongozwa vyema na nyota wao akiwemo Francis Kahata aliyeibuka mchezaji bora wa mechi hiyo huku mabao yao yakifungwa na Hassan Dilunga na Miraji Athuman ambaye sasa amefikisha mabao matatu.

Simba ambao wapo Kundi B sasa watacheza na Namungo ambao ni best looser walishinda mechi yao dhidi ya Jamhuri bao 2- 0 huku ikiizidi Mtibwa kwa mabao ambapo mabingwa hao wa zamani wana bao moja.
Yanga kutoka Kundi A yenyewe imefuzu hatua hiyo kwa kukusanya pointi nne walizozipata katika mechi mbili, walitoka sare na Jamhuri huku wakishinda dhidi ya Namungo.

Yanga watamsubiri mshindi wa kwanza kutoka Kundi C ambapo Azam FC atacheza na Malindi FC, timu hizo kila moja ina pointi moja kutokana na sare walizopata mechi zilizopita. Timu hizo zilicheza na Mlandege ambako kila timu ilitoka sare na kuifanya Mlandege kukusanya pointi mbili na kutupwa nje ya mashindano hayo.
Simba na Yanga zimeongoza makundi yao ambapo Simba imetinga hatua hiyo ikiwa na pointi sita huku Yanga wana pointi nne, watani hao kama itatokea kukutana labda ni kwenye fainali napo wakifanikiwa kuvuka hatua inayofuata.
Yanga atamsubiri mshindi kati ya Azam na Malindi kucheza nusu fainali mechi itakayochezwa leo Jumapili usiku kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja.