Mtihani wa Mangombe Tabora United

Muktasari:
- Kiazayidi aliiongoza Tabora United katika michezo 13 ya Ligi Kuu Bara, akishinda sita, kutoka sare tano na kupoteza miwili pekee dhidi ya Simba na JKT Tanzania. Aliondoka akiwa ameisaidia timu hiyo kukusanya pointi 23 kati ya 37 na sasa inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 37 katika michezo 23.
KOCHA mpya wa Tabora United, Genesis Mangombe anakabiliwa na mtihani mgumu wa kuhakikisha timu hiyo inaendelea kuwa na mwendelezo mzuri wa matokeo baada ya kuondoka kwa Anicet Kiazayidi.
Kiazayidi aliiongoza Tabora United katika michezo 13 ya Ligi Kuu Bara, akishinda sita, kutoka sare tano na kupoteza miwili pekee dhidi ya Simba na JKT Tanzania. Aliondoka akiwa ameisaidia timu hiyo kukusanya pointi 23 kati ya 37 na sasa inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 37 katika michezo 23.
Changamoto ya kwanza kwa Mangombe ni kuhakikisha anapata matokeo mazuri kwenye mchezo wake wa kwanza dhidi ya Yanga, Aprili 2, timu ambayo Tabora United tayari iliifunga 3-1 katika mzunguko wa kwanza chini ya Kiazayidi.
Hata hivyo, tofauti na mechi ya kwanza, Yanga sasa ni timu yenye ari kubwa baada ya kufanya vizuri katika michezo iliyopita wakiwa chini ya Miloud Hamdi na itakuwa na nia ya kulipa kisasi.
Kuziba pengo la Kiazayidi si kazi rahisi kwa Mangombe, hasa kwa kuzingatia kuwa aliyemtangulia alifanikiwa kuwapa Tabora United mwelekeo mzuri wa ushindani dhidi ya timu kubwa. Zaidi ya mchezo dhidi ya Yanga, Mangombe anakabiliwa na ratiba yenye changamoto kubwa ikiwamo mechi dhidi ya Pamba, Mashujaa, Singida Black Stars, KMC, Azam na Coastal Union.
Uwezo wa Mangombe kuboresha kikosi chake kwa haraka utaonekana kwa namna atakavyowapa mbinu zake mpya nyota wake.
Tabora imekuwa na safu imara ya ushambuliaji na nidhamu nzuri ya kiuchezaji, lakini utayari wa wachezaji wake kubadilika kwa haraka na kuendana na falsafa mpya ya kocha mpya utakuwa kipimo muhimu.
Katika eneo la ushambuliaji, Offen Chikola amefunga saba, Heritier Makambo (5) na Yacouba Songne (4).
Kwa kuwa tayari wameondolewa katika Kombe la FA na Kagera Sugar, msisitizo mkubwa kwa Tabora United sasa ni kuhakikisha inamaliza msimu nafasi nzuri ya Ligi Kuu.
Lengo la Mangombe linapaswa kuwa angalau kulinda nafasi ya tano au hata kupanda zaidi ikiwa wataweza kupata matokeo mazuri dhidi ya timu ngumu zilizosalia kwenye ratiba yao.
Akiongelea majukumu ambayo yapo mbele yake, Mangombe alisema; “Nipo hapa kufanya kila ambalo litakalowezekana ili kuisaidia timu kufikia malengo yake, ninachoweza kuahidi kufanya kazi kwa bidii na kundi hili la wachezaji ili kufanya vizuri kwenye kila mchezo ambao utakuwa mbele yetu.”
Katika michezo iliyopita, Tabora United imekuwa ikiruhusu mabao ambayo yanaweza kuzuiwa. Kuimarisha safu ya ulinzi dhidi ya timu kama Yanga, Azam na Coastal Union ni jambo la msingi endapo wanataka kubaki na matumaini ya kumaliza msimu kwa mafanikio.
Kingine ambacho Mangombe atakabiliana nacho ni kudhibiti presha ya wachezaji wake, hasa wakizingatia wanakabiliwa na mechi ngumu ambazo zinaweza kuathiri ari na motisha yao.