Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mudrik ana viunzi viwili Fountain Gate

Muktasari:

  • ‘Gomez’ amekuwa katika kiwango bora tangu ajiunge na timu hiyo akitokea KVZ ya Zanzibar ambapo alihusika katika jumla ya mabao 27 kupitia michezo 27, aliyocheza kati ya 30, huku akifunga mabao 20 na kuchangia mengine saba kwa kuasisti.

MSHAMBULIAJI mpya wa Fountain Gate, Mudrik Abdi Shehe ‘Gonda’ aliyetokea JKU ya visiwani  Zanzibar, licha ya kujivunia kipaji cha kutupia mipira nyavuni, lakini anakabiliwa na viunzi viwili, wakati atakapoanza kukitumikia kikosi hicho kitakachovaana na Simba leo mjini Babati, Manyara.

Kiunzi cha kwanza ni cha kuziba pengo la aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, aliyejiunga na Wydad Casablanca ya Morocco, huku kingine kikiwa ni kuzima ndoto mbaya ambayo washambuliaji wa Zanzibar wamekuwa nayo kila wanapokuja kucheza Ligi Kuu Bara.

‘Gomez’ amekuwa katika kiwango bora tangu ajiunge na timu hiyo akitokea KVZ ya Zanzibar ambapo alihusika katika jumla ya mabao 27 kupitia michezo 27, aliyocheza kati ya 30, huku akifunga mabao 20 na kuchangia mengine saba kwa kuasisti.

Hadi anaondoka nchini, Gomez alikuwa amefunga mabao sita ya Ligi Kuu huku akitengeneza pacha kali ya ushambuliaji na nyota mwenzake aliyebakia kikosini, Edgar William ambaye kwa sasa tayari ameshafunga mabao matano akiwa na kikosi hicho.

Licha ya Mudrik kuondoka Zanzibar akiwa amefunga mabao manane, rekodi zinaonyesha washambuliaji wengi kutoka Zenji wameshindwa pia kutamba wakichezea Bara, baadhi yao wakishindwa kufikisha hata mabao matano.

Miongoni mwa nyota waliotoka Zanzibar na kuja kuichezea Ligi Kuu Bara huku wakitabiriwa makubwa ni Maabad Maulid wa Coastal Union, ambaye pia alitoka akiwa mfungaji bora wa Ligi ya Zanzibar (ZPL), ila ameshindwa kufikisha hata mabao matano.

Maabad alijiunga na kikosi hicho Julai 11, 2022 akitokea KVZ ya Zanzibar ambako aliibuka mfungaji bora mara mbili mfululizo, akianza msimu wa 2020-21, alipofunga mabao 17, kisha msimu uliofuata wa 2021-22, alipofunga mabao 21.

Licha ya rekodi hiyo bora kwake, tangu amejiunga na Coastal Union hajawahi kufikisha hata mabao matano ya Ligi Kuu, kwani msimu wake wa kwanza wa 2022-23, alifunga mabao manne na msimu uliopita wa 2023-24, alifunga matatu tu.

Msimu huu pekee wa 2024-2025, tayari nyota huyo amefunga mabao manne huku bao la mwisho kufunga lilikuwa la kichapo cha timu hiyo cha mabao 3-2, dhidi ya Fountain Gate alilolifunga dakika ya 79, mechi ikipigwa Babati Desemba 13, mwaka jana.

Mbali na Maabad, nyota mwingine ni Yassin Mgaza ambaye pia alikuwa mfungaji bora katika Ligi ya Zanzibar (ZPL) akiwa na kikosi cha KMKM msimu wa 2022-23, ambapo alifunga mabao 17 na kuasisti manane kupitia michezo 25 aliyocheza.

Kwa maana yake, Mgaza alihusika katika mabao 25 akiwa na timu ya KMKM kupitia michezo 25 aliyocheza kati ya 30 kwa msimu mzima ikiwa ni msimu wake wa kwanza tu kucheza Ligi ya Zanzibar na kuwavutia mabosi wa Dodoma Jiji kumsajili kikosini.

Mgaza alijiunga na KMKM akitokea Mbuni ya Arusha ambayo kwa sasa inashiriki Ligi ya Championship ingawa kwa msimu huo ilikuwa Ligi Daraja la Pili, First League, ambapo alionyesha kiwango kizuri kilichoishawishi KMKM kuihitaji saini yake.

Akiwa na kikosi cha Mbuni, Mgaza alihusika katika jumla ya mabao 22 kwa msimu mzima kwenye michezo 16, aliyocheza baada ya kufunga 16 na kuasisti mengine sita, akiendeleza kiwango chake bora hadi alipojiunga pia na timu ya KMKM.

Baada ya hapo mabosi wa Dodoma Jiji wakamsajili kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji kwa msimu wa 2023-2024 na kubeba matarajio makubwa ndani ya kikosi hicho ingawa aliangukia pua baada ya kufunga mabao matatu tu msimu mzima.

Msimu huu wa 2024-25, Mgaza amefunga bao moja tu lililokuwa la kichapo ilichokipata Dodoma Jiji cha mabao 2-1, dhidi ya Singida Black Stars, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, uliopigwa Uwanja wa CCM Liti Singida, Desemba 12, mwaka jana.

Ukiangalia rekodi hiyo kwa miaka ya hivi karibuni, unaona washambuliaji wengi waliotokea Zanzibar wameshindwa kuwika katika Ligi Kuu Bara.