Mwalwisi akomalia Top Four Mbeya Kwanza

Muktasari:
- Mwalwisi aliyejiunga na kikosi hicho akitoka TMA FC ya jijini Arusha aliyoiongoza katika michezo 15 ya raundi ya kwanza, alisema ushindani ni mkubwa hasa mechi za mwishoni, ingawa amejipanga kuhakikisha wanaishi kwenye malengo waliyojiwekea.
KOCHA wa Mbeya Kwanza, Maka Mwalwisi amesema kikosi hicho bado kina nafasi ya kumaliza nafasi nne za juu 'Top Four' kwa michezo iliyobakia, huku akiwataka wachezaji wa timu hiyo kuendelea kupambana na kutokata tamaa hadi mwishoni mwa msimu huu.
Mwalwisi aliyejiunga na kikosi hicho akitoka TMA FC ya jijini Arusha aliyoiongoza katika michezo 15 ya raundi ya kwanza, alisema ushindani ni mkubwa hasa mechi za mwishoni, ingawa amejipanga kuhakikisha wanaishi kwenye malengo waliyojiwekea.
"Malengo yetu ni kuendelea kupigania nafasi mbili za juu au ikishindikana tumalize ndani ya nne bora, hilo linawezekana kwa sababu gepu la pointi na washindani wetu sio kubwa, jambo la muhimu ni kuongeza umakini kwa kila mchezo," alisema.
Kocha huyo amejiunga na Mbeya Kwanza akichukua nafasi ya Emmanuel Masawe na hadi sasa ameiongoza katika michezo tisa na kati ya hiyo ameshinda minne, sare mitatu na kupoteza miwili na amefunga jumla ya mabao 15 na kuruhusu manane tu.
Kijumla timu hiyo imecheza michezo 24 hadi sasa, ikishinda 12, sare sita na kupoteza pia sita, inashika nafasi ya sita na pointi zake 42, huku eneo la ushambuliaji likifunga mabao 33 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 22.