Mwembe Makumbi yarejea kileleni, Mlandege ikifanya mauaji ZPL

Muktasari:
- Mwembe Makumbi imerejea nafasi ya kwanza katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) baada ya kuifunga Chipukizi bao 1-0 na kufikisha pointi 49, huku Mlandege ikiifanyia mauaji Tekeleza kwa kuitembezea kichapo cha mabao 11-1 ikirejea nafasi ya pili.
TIMU ya Mwembe Makumbi City, imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) baada ya kuitandika Chipukizi bao 1-0 katika mchezo uliofanyika leo Jumapili Mei 18,2025 kwenye Uwanja wa Finya uliopo kisiwani Pemba.
Mwembe Makumbi ambayo ilikaa kileleni kwa takribani miezi minne kabla ya kushushwa na Mafunzo hatimaye, imerejea katika nafasi hiyo baada ya Robert Pius kuipatia bao pekee dakika 82.
Katika mchezo mwingine uliopigwa leo kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja, Mlandege imewafanyia mauaji Tekeleza kwa kuitandika mabao 11-1.
Tekeleza ambayo tayari imeshuka daraja na msimu ujao ikitarajiwa kushiriki Ligi Daraja la Kwanza, ilijikuta ikikutana na dhahama hiyo nzito bila kutarajia.
Abdalla Iddi 'Pina' amefunga mabao saba peke yake huku Said Matola 'Kunguru' akifunga mawili, wakati Mahmoud Mkonga na Mohamed Ali wakifunga bao moja moja kuhitimisha ushindi huo mnono.
Kwenye Uwanja wa Mao B, Unguja, Uhamiaji na Mwenge wametoka sare ya bao 1-1.
Michezo ya leo imezifanya timu ya Mlandege kuvuna alama 47, huku Mwembe Makumbi ikifikisha alama 49 na kukaa kileleni mwa msimamo.
Ligi hiyo itaendelea kesho Jumatatu ambapo Zimamoto itavaana na InterZanzibar kwenye Uwanja wa Mao B na KMKM itakutana na Kipanga, Uwanja wa Mao A.