Mzunguko wa 21 ZPL, furaha, vilio na migongano
Muktasari:
- Tangu Septemba 25, 2025 ulipoanza msimu huu, ligi hiyo imekuwa na mfululizo wa matukio mbalimbali ikiwamo kupigwa waamuzi kwa madai ya kuchezesha wakiwa na matokeo yao mkononi, jambo ambalo linaharibu taaswira ya soka visiwani hapa.
MZUNGUKO wa 21 wa Ligi Kuu Zanzibar umemalizika kwa kuacha furaha na majeraha kwa baadhi ya timu huku zingine zikiwa na vilio kwa kunyimwa haki zao.
Tangu Septemba 25, 2025 ulipoanza msimu huu, ligi hiyo imekuwa na mfululizo wa matukio mbalimbali ikiwamo kupigwa waamuzi kwa madai ya kuchezesha wakiwa na matokeo yao mkononi, jambo ambalo linaharibu taaswira ya soka visiwani hapa.
Kocha wa Fufuni, timu iliyopanda daraja msimu huu kutoka Pemba, Suleiman Mohamed ‘Mani Gamera’ amesema kikosi hicho kimekumbwa na kadhia ya kunyimwa haki zake katika mechi iliyochezwa Alhamisi April 2, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A, uliopo Mjini Unguja, ambapo ikajikuta ikipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Polisi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mani Gamera alisema ushindi walioupata Polisi katika mechi hiyo haukuwa wa halali akidai kikosi chake kunyimwa penalti mbili na mwamuzi wa kati, Rashid Shahran ‘Webu’ ambazo zilikuwa halali.
“Kwanza nilishangazwa na mambo mengi kwenye mechi ya juzi ikiwemo Polisi kuchezesha kipa aliyeoneshewa kadi nyekundi, Said Suleiman ‘Diego’ kwenye mechi ya JKU dhidi ya Polisi, la pili kutunyima penalti mbili wakati ilikuwa haki yetu,” alisema kocha huyo.
Mechi hiyo ya JKU dhidi ya Polisi ilichezwa Ijumaa Februari 13, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A, uliopo Unguja saa 10:15 jioni.
Mani Gamera alieleza kuwa, Mwamuzi Webu hakuwa sahihi kufanya uamuzi huo, ingawa amekiri vitu vya aina hiyo hutokea katika mpira wa miguu, lakini vinapozidi vinakuwa karaha kwa sababu vinashusha hadhi ya mchezo huo.
“Kama amefanya hivyo kwa kupewa maagizo kutoka kwa mtu au kikundi cha watu kuharibu mpira ni sawa, ikiwa uamuzi huo uliotokana na sheria 17 za mpira kuwa hivyo, kwa kweli wanaukosea mpira,” alisisitiza Mani Gamera.
Kocha huyo, alisema awali Fufuni walikuwa na malengo ya kupambana msimu wa kwanza kutoshuka daraja, lakini baada ya kuona wanaweza kupambania ubingwa ndipo wakabadili malengo na kuwania ubingwa kwani hilo ndio jambo muhimu kuliko yote.
Mani Gamera alisema timu hiyo ipo tayari kupambana na yeyote anayetaka kuwaharibia malengo yao kwani anaona wapo ambao wameshakula viapo kuwa Fufuni haitochukua ubingwa wala kumaliza msimu kwenye nne bora.
Mani Gamera ametoa wito kwa timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Zanzibar kujipanga mapema ili wasishuke daraja kama walivyofanya timu yao hapo awali ikiwemo kuzifunga timu kongwe kama KVZ, Uhamiaji, Zimamoto na Kipanga.
Alisema, hakuna aliyetarajia kuwa timu hiyo itatoa ushindani wa namna hiyo kwenye ZPL lakini imetokea kwa namna ilivyojipanga kupambana.
Alifichua kwamba, mzunguko huu wa pili timu hiyo imekuwa bora zaidi ya mzunguko wa kwanza, hivyo anahitaji kuachwa kufanyakazi yake na wengine wafanye kazi zao.
Vilevile, kocha huyo ametoa wito kwa viongozi pamoja na mashabiki wa soka Zanzibar kuacha dhana ya kuamini kuwa mpira upo kwenye timu za vikosi pekee na sio kiraia.
“Baadhi ya viongozi wa mpira wanaamini kwamba mpira upo Unguja, ila Pemba hakuna mpira jambo ambalo sio kweli. Tunatamani hata Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi alitambue hili kwa sababu haya yanaumiza,” alisema Mani Gamera.
Alisema kipindi hiki unapowavunja mioyo wachezaji inakuwa kazi ngumu kwa kocha kuwarudisha kwenye hali za kawaida hususan kwa timu ya Fufuni ambayo inajiendesha yenyewe kupambania matokeo mazuri.