Ntibazonkiza atupia mbili, Yanga kicheko tu

KIRAKA Saido Ntibazonkiza ameanza vyema katika kikosi cha Yanga baada ya kutupia mabao mawili katika mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Singida UTD uliomalizika wakishinda 3-0 katika uwanja wa Liti.
Katika mchezo huo Saido alionekana kuwa bora zaidi katika umiliki wa mpira na kuwafanya mabeki wa Singida wahahe.

Mchezaji huyo pia alikuwa bora katika kutengeneza nafasi kwa wachezaji wenzake lakini umakini wao katika kumalizia ulionekana kuwa changamoto.
Dakika 22 Saido Ntibazonkiza aliifungia Yanga bao la kwanza baada ya kupokea pasi kwa Farid Mussa na yeye aliuchopu mpira juu ya mabeki wa Singida na kukimbia na mpira kisha akaupiga mpira na kwenda moja kwa moja wavuni.

Baada ya kupata bao hilo Yanga walionekana kuhaha zaidi kupata bao lingine, lakini walikuwa wanakumbana na changamoto ya mabeki wa Singida.
Dakika 65 Ntibazonkiza aliifungia Yanga bao la pili kwa mkwaju wa penalti, baada ya Waziri Junior kumipigia pasi Ditram Nchimbi na kufanyiwa madhambi ndani ya boksi.
Dakika 85 Ntibazonkiza alitolewa na nafasi yake ilichukuliwa na Deus Kaseke ambaye alitumia dakika moja tu (dakika 86) kuifungia Yanga bao la tatu baada ya kupigiwa pasi na Adeyum Saleh na yeye kuonganisha mpira moja kwa moja.
Singida imekuwa na historia nzuri kwa wachezaji wanaosajiliwa na Yanga kwani mshambuliaji Yikpe alianza kutupia bao la kwanza tangu ajiunge Yanga, Bernard Morrison mechi ya kwanza aling’aa kwa kutoa assisti kisha kupanda mpira na leo Ntibazonkiza ametupia mbili mechi ya kwanza.
KAZE AFUNGUKA
Kocha mkuu wa Yanga, Cedric Kaze amesema kiwango alichokionyesha mchezaji wake anakifurahia kwani ameongeza kitu katika timu yake.
"Saido ni mchezaji mzuri na ameongeza kitu kwenye kikosi, ni mchezaji kiongozi na ameongoza vyema wachezaji wenzake."
Akizungumzia mchezo kiujumla, alisema mchezo huo ametumia kuwapa nafasi wachezaji ambao wamekuwa hawapati nafasi.

"Hii ni mechi ambayo kwa wale wanakosa muda wa kucheza kupata muda na wao ili kuwa bora," amesema Kaze
Imeandikwa na Thomas Ng'itu