Nyambaya aendelea kumwaga vifaa

KLABU tatu za kutoka Mkoa wa Dar es Salaam zimekabidhiwa vifaa tayari kwenda katika kushiriki Mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa.
Klabu ambazo zimepewa msaada huo ni Mabomba FC inayokwenda kituo cha Lindi, Huduma SC itakayokuwa kituo cha Arusha na Temeke Squad itakayotua Pwani katika mashindano yatakayoanza Machi 4 mwaka huu.
Vifaa hivyo vimetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Lameck Nyambaya akizitaka klabu hizo kwenda kuhakikisha zinaupa heshima mkoa huo.
Katika makabidhiano hayo Nyambaya ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendai ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) amesema dhamira yake ni kutamani kuona klabu za kutoka jiji hilo zinakuwa na ushiriki mzuri katika mashindano hayo.
Mbali na vifaa hivyo vikiwemo jezi seti moja kwa kila timu na mipira pia Nyambaya amezikabidhi kila timu kiasi cha sh 300,000 zikazowasaidia katika maisha yao kwenye vituo vyao.
"Huu ni mkoa mkubwa na sisi kama viongozi tunatakiwa kuhakikisha klabu hizi ambazo zinatoka katika maeneo yetu zinakuwa sio kwenda kushiriki bali zinashindana na kuleta heshima ndani ya jiji hili,"amesema Nyambaya.
"Nataka mwende huko mkalete ushindi na sio kushindwa hiki ninachofanya kwenu kikawe chachu ya kutafuta ushindi kwa kila mchezo,sisi viongozi tumetekeleza wajibu wetu kazi kwenu huko mnakokwenda."
Huu umekuwa kama muendelezo wa Nyambaya kwani hivi karibuni alizipa vifaa mbalimbali timu za Veterans ambao ni wachezaji wa zamani wa timu za ligi kuu kutoka katika mkoa huo.