Pamba Jiji yaanza kujipanga, yatangaza bodi yake

Muktasari:

  • Juni 19 mwaka huu Pamba Jiji ilitangaza kumalizika kwa mikataba ya benchi lake la ufundi lilioipandisha timu hiyo Ligi Kuu, tangazo ambazo lilitolewa siku nne tu tangu TP Lindanda imtangaze Goran Kopunovic kubeba mikoba ya kocha Mbwana Makata aliyeipandisha daraja.

Zikiwa zimepita siku 10 tangu Klabu ya Pamba Jiji itangaze kumalizika kwa mikataba ya benchi la ufundi na wachezaji walioipandisha Ligi Kuu, klabu hiyo imetangaza bodi mpya itakayoiongoza kwa kipindi cha miaka mitano.

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi Juni 29, 2024, na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba ambaye ni Katibu wa Bodi hiyo huku akimtaja mwenyekiti wa bodi hiyo kuwa ni Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Costantine.

Kibamba amesoma majina ya viongozi wengine wa bodi ya timu hiyo inayomilikiwa na Jiji la Mwanza kuwa ni mwanasheria wa timu, Triphonia Kisiga na Jeremiah Lubeleje ambaye ni Ofisa Mipango wa Jiji ambaye atatekeleza wajibu huo wa Ofisa Mipango katika timu hiyo.

Nafasi ya ofisa michezo wa timu atakuwa, Joseph Masele wakati Ngollo Mussa anakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma, huku wajumbe wa kuteuliwa wakiwa ni Jamal Babu, Mwita Gachuma, Evarist Hagila, Vedastus Rufano, Msema Kawewe, Bob Butambala na Alhaji Majogoro.

Kwa upande wa wateuliwa katika kamati ya utendaji ni mwenyekiti wa timu, Bhiku Kotecha, Ezekiel Nyangoma (meneja wa timu), Martin Sawema (ofisa habari), Noel Kingu (mtunza vifaa), Joseph Chacha (daktari wa timu), Agness Magubu (ofisa utamaduni) na Regan Kisima (mhasibu) huku ofisa mtendaji mkuu wa timu akitarajiwa kuajiriwa na bodi.

Kwenye kamati ya mashindano, Pamba Jiji imemtangaza, Mohamed Bitegeko kuwa mwenyekiti, Jafari Juma (katibu) na wajumbe ni Agness Magubu, Calvin Chera, Nyangoma Ntibijeha na Fura Felician.

Wakati huo, kamati ya nidhamu ya klabu hiyo itaongozwa na Alhaji Majogoro (mwenyekiti), Rehema Mdoe (katibu) huku wajumbe wakiwa ni Paresh Kotecha, Fumo Felician, Khalfan Ngassa, Sophia Makilagi na Aleem Alibhai.

“Viongozi hawa tumewapata kwa kuzingatia sababu mchanganyiko kwa sababu wamiliki wa timu ni Halmashauri kwa maana kwamba Pamba Jiji ni timu ya wananchi. Kwa hiyo uongozi huu umezingatia, wananchi, maveteran na viongozi walioipandisha timu kwa nyakati tofauti,” amesema Kibamba.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ambaye ni mlezi wa klabu hiyo amewataka viongozi wa bodi hiyo kuzingatia demokrasia na kuepuka migogoro huku akidokeza kuwa tayari menejimenti ya jiji hilo imepitisha bajeti ya zaidi ya Sh1.5 bilioni kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa timu hiyo.

“Mara nyingi sana kwenye mambo ya michezo kuna fitna nyingi sana huyu akae hapa, yule awe nani na huyu awe nani, hii ni timu yetu sote na wana Mwanza watapata fursa ya kuitumika Pamba Jiji awamu kwa awamu kwa hiyo bodi ya timu muda wenu utakapoisha mkubali kuachia kijiti. Hii timu siyo ya mtu ni yetu tunawajibu wa kuilea ifanye vizuri zaidi,” amesema Mtanda.

Mtanda amesema; “Tunaendelea kuunda nafasi za uongozi kwa ambao hawajapata nafasi sasa hivi wataipata baadaye, bodi ifuate kalenda ya vikao, kufanya uamuzi kwa haki na demokrasia, kuzingatia maslahi ya Pamba na wananchi, na kutovunja katiba.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Pamba Jiji, Sima Costantine amesema dhamira ni kuhakikisha Pamba Jiji inarejesha makali yake kupitia usimamizi bora ili kurejesha burudani ya soka jijini humo.

“Tuko tayari kuanza utekelezaji wa majukumu tuliyokasimiwa kwa mujibu wa Katiba tuliyoizindua leo, tuonane Ligi Kuu,” amesema Sima.

Kwa mujibu wa Mjumbe wa Kamati ya Nidhamu, Sophia Makilagi, uteuzi wake katika wadhifa huo ni ishara ya Pamba Jiji kuamini katika usawa huku akiahidi uwajibikaji utakaoiwezesha kusalia Ligi Kuu na kuleta ushindani kwa timu kongwe katika ligi hiyo.