Rekodi inavyoihukumu JKT Tanzania
Muktasari:
- Katika mechi ya mwisho ya msimu wa Ligi Kuu ya NBC iliyochezwa Juni 30, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar wakati Yanga ikishinda kwa mabao 3-0, Wahabi alimchezea madhambi Pacome dakika ya 46 na kushindwa kuendelea na mechi hiyo iliyoipa Yanga taji la tano mfululizo. Majeraha hayo yamemfanya Pacome afanyiwe upasuaji na kutarajiwa kukaa nje kwa wiki sita.
WAKATI uongozi wa JKT Tanzania ukiguswa na kuomba radhi kwa mashabiki wa soka baada ya mchezaji wa timu hiyo, Hassan Wahabi kumfanyia rafu mbaya kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua, rekodi zinawahukumu wachezaji wa kikosi hicho, kwani tangu kuanza msimu wa 2024-2025, hadi 2025-2026, ndiyo wanaoongoza kwa kuonyeshwa kadi nyekundu.
Katika mechi ya mwisho ya msimu wa Ligi Kuu ya NBC iliyochezwa Juni 30, 2026 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar wakati Yanga ikishinda kwa mabao 3-0, Wahabi alimchezea madhambi Pacome dakika ya 46 na kushindwa kuendelea na mechi hiyo iliyoipa Yanga taji la tano mfululizo. Majeraha hayo yamemfanya Pacome afanyiwe upasuaji na kutarajiwa kukaa nje kwa wiki sita.
Wachezaji wa JKT Tanzania wameonyeshwa kadi nyekundu sita za Ligi Kuu ya NBC, wakifuatiwa na TRA United na Pamba Jiji ambazo kila moja zimepata nne na KMC tatu.
Nyota wa kwanza kuonyeshwa kadi nyekundu kwa JKT ni kipa Denis Richard katika kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Yanga, Oktoba 22, 2024.
Nyota mwingine ni Mohamed Bakari, katika kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Simba, lililofungwa kwa penalti na Jean Charles Ahoua dakika ya 90+5, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Desemba 24, 2024.
Msimu huu wa 2025-2026, nyota wanne wameonyeshwa kadi nyekundu, akianza pia kipa Ramadhan Chalamanda dhidi ya Mbeya City, Oktoba 24, 2025, katika sare ya 2-2.
Mwingine ni Salum Khamis katika kichapo bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Januari 30, 2026, huku beki wa kushoto, Karimu Mfaume alionyeshwa katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa, Februari 9, 2026 kabla ya Wahab kufanya hivyo, Jumanne iliyopita.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amesema hakuna mchezaji anayedhamiria kumuumiza mwingine, isipokuwa ni makosa ya kimchezo yanayotokea uwanjani, hivyo haina maana wachezaji hao wanakosa nidhamu ya kiuchezaji.