Prime
Rekodi zaibeba Simba Amaan

Muktasari:
- Wakati Simba itatumia uwanja huo kwa sababu ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam umefungiwa na Serikali, inaelezwa kuwa Simba haina rekodi mbaya Amaan pia wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa ligi uliopigwa Septemba 26 mwaka jana.
BAADA ya Simba kutanganza kuwa mechi yao dhidi ya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini itachezwa kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar, wadau wa soka wameitaka kujiandaa vizuri ili kutumia vizuri uwanja huo kwa kupata mabao ya kutosha, huku dimba hilo haliwajawahi kuwapa matokeo mabaya.
Wakati Simba itatumia uwanja huo kwa sababu ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam umefungiwa na Serikali, inaelezwa kuwa Simba haina rekodi mbaya Amaan pia wakiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa ligi uliopigwa Septemba 26 mwaka jana.
Simba itakuwa mwenyeji wa Stellenbosch FC ya Afrika Kusini mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Aprili 20 mwaka huu kabla ya kurudiana Aprili 27 nchini Afrika Kusini. Mshindi wa jumla baina yao atatinga moja kwa moja katika hatua ya fainali.
Hata hivyo, Simba licha ya kuwa huo utakuwa ni mchezo wake wa kwanza wa kimataifa kwenye uwanja huo ina uzoefu na uwanja huo kwenye michuano ya Mapinduzi ambayo wametwaa taji mara sita, lakini pia kwa msimu huu kwa mechi za CAF haijapoteza mchezo wowote nyumbani.
Ilianzia raundi ya pili na kushinda mabao 3-1 dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya na katika makundi ilishinda dhidi ya Bravos ya Angola kwa bao 1-0, kisha kuinyoa Sfaxien ya Tunisia kwa mabao 2-1 na kuilaza pia Cs Constantine kwa mabao 2-0 na hatua ya robo fainali iliinyoa Al Masry kwa mabao 2-0 kisha kupigiana penalti na Wekundu hao kuibuka na ushindi wa 4-1 na sasa ni zamu ya Stellenbosch.
Mashindano hayo yalianzishwa mwaka 2007, ambao mabingwa wa michuano hiyo, kinara akiwa Azam FC imechukua (5) Simba (nne), Yanga (mbili), Mtibwa Sugar (mbili), wakati Miembeni ya Zanzibar (moja), URA (moja) na KCCA (moja) na Mlandege (moja).
WASIKIE WADAU
Ulimboka Mwakingwe nyota aliyeisaidia Simba SC kufika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003 kwa kuwatoa waliokuwa mabingwa watetezi, Zamalek amewataka Simba kujiandaa vizuri kwani popote wanaweza kushinda.
“Ili upate ushindi katika mechi hatua ya mtoano lazima ujiandae vizuri kwani hata ubadilishe uwanja kama huna maandalizi ni kazi bure naamini Simba ina uzoefu mkubwa na Uwanja wa Amaan ikijiandaa vyema inaweza kutumia vizuri uwanja huo bila kujali kwamba kimataifa wao pia ni wageni kutokana na kutocheza mchezo wowote kwenye uwanja huo,” alisema Ulimboka na kuongeza;
“Simba ina timu nzuri, hatua waliyopo sio ya kutokutumia nafasi wanazotengeneza wanachotakiwa kufanya ni kuwa makini kwenye eneo lao la ushambuliaji. Wapambane washinde mechi hiyo nyumbani kwani kwenye michuano hii kila mmoja anaamini kwenye uwanja wake wa nyumbani naamini wakijiandaa vizuri wana nafasi kubwa ya kutinga hatua inayofuata.”
Kocha wa zamani wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, Boniface Mkwasa alisema Simba wanatakiwa kupata mabao ya kutosha katika mchezo huo ili kujitengenezea mazingira mazuri katika mchezo wa marudiano bila kujali wanacheza kwenye uwanja gani japo ni kweli imezoeleka kuwa wao kwa Mkapa hatoki mtu anaamini hiyo kauli bila maandalizi hakuna kitu.