Simba yaipeleka Stellenbosch Zenji

Muktasari:
- Simba itavaana na timu hiyo ya Afrika Kusini Jumapili ya wikiendi hii kwenye Uwanja wa Amaan Complex, baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kufungiwa kwa muda kupisha ukarakati na mabosi wa Msimbazi wameamua kuuchagua uwanja huo wa uliopo mjini Unguja.
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya CAF, Simba imeamua kuwapeleka wapinzani wao wa mechi za nusu fainali, Stellenbosch ya Afrika visiwani Zanzibar.
Simba itavaana na timu hiyo ya Afrika Kusini Jumapili ya wikiendi hii kwenye Uwanja wa Amaan Complex, baada ya Uwanja wa Benjamin Mkapa kufungiwa kwa muda kupisha ukarakati na mabosi wa Msimbazi wameamua kuuchagua uwanja huo wa uliopo mjini Unguja.
Mchezo huo wa hadhi kubwa umepangwa kuanza saa 10:00 jioni. Uamuzi wa kubadilisha uwanja umetokana na agizo la Serikali la kusitisha kwa muda shughuli zote za soka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kuruhusu ukarabati wa dharura, hasa kwenye mfumo wa mifereji ya maji ya mvua.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia tukio la sintofahamu lililotokea wakati wa mechi ya marudiano ya robo fainali dhidi ya Al Masry ya Misri, ambapo mvua kubwa ilinyesha na kuonesha upungufu mkubwa kwenye mifereji ya uwanja huo. Eneo la kuchezea lilijaa maji kiasi cha kuwafanya wahudumu wa dharura kutumia magodoro kujaribu kufyonza maji na kurejesha hali ya uwanja.
Baada ya tukio hilo, serikali ilitoa tamko la kusitisha matukio yote yaliyopangwa kufanyika katika uwanja huo na kuwaagiza vilabu vyote, ikiwemo Simba, kutafuta viwanja mbadala kwa ajili ya michezo yao inayofuata.
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ilisisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto za miundombinu ili kuhakikisha Uwanja huo unakidhi viwango vya kimataifa kwa siku zijazo.

Chanzo cha kuaminika kimethibitisha kuwa Simba kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wamechagua Uwanja New Amaan Complex uliopo Zanzibar kama Uwanja mbadala unaofaa zaidi.
Maandalizi yako kwenye hatua nzuri, na uwanja huo umeshafanyiwa ukaguzi na kupitishwa kwa ajili ya kuandaa mchezo wa kiwango cha juu kama huu.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, ujumbe ulioongozwa na kiongozi wa Simba, Abbas Ally, pamoja na wawakilishi wengine wa klabu hiyo, walifanya mazungumzo yenye mafanikio na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF).

Mazungumzo hayo yalijumuisha ukaguzi wa kina wa Uwanja na makubaliano ya mipango ya kiufundi na kiutawala ili kuhakikisha vigezo vyote vinavyotakiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) vinatimizwa.
Chanzo hicho kimeongeza kuwa makubaliano rasmi yamefikiwa kati ya uongozi wa Uwanja na klabu, na mechi itachezwa kama ilivyopangwa awali.
Wapinzani wa Simba kwenye nusu fainali, Stellenbosch, tayari wamejulishwa rasmi kuhusu mabadiliko ya Uwanja na wanatarajiwa kuwasili Zanzibar siku mbili kabla ya mechi ili kuzoea mazingira na kukamilisha maandalizi ya mwisho.
Kufanyika kwa mechi muhimu ya nusu fainali ya CAF huko Zanzibar ni fursa adimu na ya kusisimua kwa mashabiki wa soka visiwani kushuhudia soka la kimataifa kwa ukaribu.

Uwanja wa New Amaan Complex, ambao umefanyiwa ukarabati mkubwa ili kufikia viwango vya kimataifa, uko tayari kabisa kwa ajili ya kuandaa mechi ya aina hii.
Mashabiki wa Simba kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania, wakiwemo wa Zanzibar, wanatarajiwa kusafiri kwa wingi kuishangilia timu yao ambayo inalenga kupata ushindi muhimu katika mechi ya kwanza kabla ya kuelekea Afrika Kusini kwa mchezo wa marudiano wiki inayofuata.