Simba, Yanga kila mtu na wake CAF

HATIMAYE wamefahamika wapinzani wa Simba na Yanga kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Wananchi watavaana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini huku Mnyama akipewa kwa mara nyingine tena, Al Ahly.
Katika droo hiyo ambayo imechezeshwa leo jioni huko Misri huku ikiongozwa na Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Samson Adamu, Simba ndio waliokuwa wa kwanza kuwafahamu wapinzani kabla ya Yanga kufuata baadaye.
Hii itakuwa mara ya pili kwa Simba kukutana na Al Ahly ndani ya msimu mmoja, ikumbukwe mwanzoni mwa msimu timu hizo zilikutana kwenye ufunguzi wa michuano mipya ya African Football League, mchezo wa kwanza Mnyama akitoka sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Mkapa huku walipoenda Misri wakitoka tena sare ya bao 1-1.
Safari ya Mnyama kwenye michuano hiyo iliishia hapo licha ya matokeo ya jumla kuwa sare ya mabao 3-3, waliondolewa kutokana na idadi kubwa ya mabao ambayo aliruhusu akiwa nyumbani.
Ka upande wa Yanga mara ya mwisho kukutana na Mamelodi ilikuwa miaka 23 iliyopita ambapo ilikuwa katika raundi ya pili ya michuano hiyo.
Yanga ilishindwa kufua dafu, ikiwa Afrika Kusini ilipoteza kwa mabao 3-2 na ikiwa nyumbani ililazimishwa sare ya mabao 3-3.
Mechi za mkondo wa kwanza zitapigwa kati ya Machi 29-31 na kurudiana kati ya Aprili 5-7, 2024.Simba na Yanga wataanzia nyumbani kwenye michezo hiyo huku wakiwa na kibarua kizito mbele yao cha kumalizia ugenini.
Wakati Simba na Yanga zikiwa na kazi ya kufanya kweli kwenye hatua hiyo, mechi nyingine za robo fainali ni kati ya TP Mazembe ya DR Congo dhidi ya Petro Atletico ya Angola na Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
NUSU FAINALI
Esperance/ASEC vs Yanga/Mamelodi
TP Mazembe/Petro Atletico vs Simba/Al Ahly
WASIKIE MAKOCHA
Mchezaji wa zamani wa Simba ambaye pia ni kocha, Julio Kihwelo amesema droo hiyo kwa upande wake imekuwa ya haki na ni sawa kwa timu hizo kubwa nchini kupangiwa wakubwa wenzao.
"Ligi yetu imekua. Iko nafasi ya tano Afrika, hivyo ukubwa huo unatakiwa uonekane kwa kucheza na timu kubwa ili kuweza kujipima vizuri, " amesema na kuongeza kwamba:
"Kama wangepangwa na vibonde, basi wasingecheza kwa ubora walionao, hivyo hakuna haja ya kuogopa chochote kwani mpira ni mchezo wa makosa sio rekodi."
Kocha wa Ihefu, Mecky Maxime ameeleza kuwa anauona ugumu kwa wababe hao wa Tanzania kwani kitendawili kikuu upande wake ni kwmba watavukaje hatua hiyo.
"Ni droo ngumu kwa timu zote. Hatua mbaya zaidi zinaanzia nyumbani. Wanakwenda kukutana na timu ambazo sasa zipo kwenye ubora mkubwa," amesema Maxime na kuongeza:
"Wanatakiwa kujipanga wasidhani na huko watawafunga tano kama wanavyoifunga Ihefu. Watafungwa wao."
Katika hatua nyingine droo ya robo fainali upande wa Kombe la Shirikisho Afrika imepangwa ambapo Future itavaana na ndugu zao wa Wamisri, Zamalek, huku Abu Salim ya Libya itacheza dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Nayo Rivers United ya Nigeria itakuna na USM Algers ya Algeria huku Stade Malien ya Mali ikipangwa na Dreams FC ya Ghana.
NUSU FAINALI
Rivers United/USM Alger vs Abu Salim/RS Berkane
Future/Zamalek vs Stade Malien/Dreams