SPOTI DOKTA: Pombe inavyoathiri utimamu wa wanasoka wetu

Muktasari:

Kwani hujaona wachezaji wengi tu wanaumia, lakini muda wao wa kurejea uwanjani umekuwa mrefu kupitiliza? Pengine moja ya sababu ni unywaji wa pombe.

KAMA mchezaji au mfanyamazoezi umewahi kujua kama unywaji pombe si salama kwako kwa upande wa kiwango chako cha uchezaji na utimamu wa mwili wako?

Kama ulikuwa hujui, kwa jumla unywaji pombe unaathiri kiwango cha mchezaji na utimamu wa mwili wake kwa njia mbili zifuatazo.

Njia ya kwanza ni kwa sababu pombe huchochea figo kuruhusu maji kupotea kwa wingi kwa njia ya mkojo, hivyo unywaji wa pombe uliopitiliza unasababisha upungufu wa maji mwilini.

Kwa mfano mwanamichezo au mchezaji akinywa pombe kwa wingi na kisha akaingia katika zoezi au mechi, anakuwa katika hali mbaya zaidi kutokana na ukweli kuwa atapoteza maji mengi kwa njia ya jasho kwa kuwa kadiri anavyocheza ndivyo joto la mwili hupanda na hivyo jasho hutoka kwa wingi.

Muunganiko wa kutokwa jasho na athari ya pombe ya kupoteza maji kwa njia ya mkojo huweza kuleta upungufu wa maji mkubwa kwa mchezaji jambo ambalo lazima litaathiri utendaji wake wa kazi uwanjani.

Wakati wote mwanamichezo hutakiwa kuwa na kiasi cha maji ya kutosha mwilini ili kuwezesha mtawanyiko mzuri wa damu. Ikumbukwe kuwa damu ndiyo imebeba oksijeni na virutubisho muhimu kwa ajili ya misuli kukunjuka na kujikunja.

Hivyo basi upungufu wa maji mwilini huathiri utendaji wa misuli hivyo, moja kwa moja huaathiri kiwango cha uchezaji na utimamu wa mwili kiujumla.

Hali ya upungufu wa maji mwilini huambatana na hali ya kubanwa misuli na kupata vijeraha vya misuli kirahisi. Vile vile kama kuna majeraha huchelewa kupona.

Kwani hujaona wachezaji wengi tu wanaumia, lakini muda wao wa kurejea uwanjani umekuwa mrefu kupitiliza? Pengine moja ya sababu ni unywaji wa pombe.

Njia ya pili ni kuwa pombe huingilia mfumo wa utengenezaji nishati ya mwili (glucose). Ikumbukwe kuwa glucose ndiyo kama petroli ya mwili inayotumiwa na misuli ya mwili kufanya kazi yake.

Pale unapokunywa pombe na inapoingia tumboni na kuvunjwa vunjwa au kusagwa huwa ini linashindwa kutengeneza kiasi cha kutosha cha nishati (glucose).

Hali hii ndiyo inayosababisha kuwa sukari ya mwili au nishati (glucose) katika damu kuwa chini. Mazoezi yoyote huitaji kiasi cha kutosha cha sukari/nishati ili kukupa nguvu.

Hivyo kwa mnywaji wa pombe ini lake hushindwa kutengeneza sukari/nishati hivyo mwili kukosa nguvu na hii huathiri kiwango cha mchezaji kwani atashindwa kucheza kwa nguvu.

Njia hizi mbili ndizo zina matokeo ambayo humsababishia mwanamichezo kukosa nguvu, misuli kuumwa na kuwa dhaifu, kuwa mchovu, kushindwa kuwa makini uwanjani, kukosa utulivu, kichwa kuuma, kubadilika tabia ikiwamo ukali au ukorofu na kuongezeka uzito kiholela.

Pia, pombe inasababisha protini tunayoipata kwa kula vyakula kutonyonywa katika mfumo wa chakula. Kukosekana kwa kirutubisho hiki kwa mwanamichezo husababisha misuli yake kushindwa kujengeka na kuimarika.

Vile vile protini ndiyo inayochangia misuli kujikunja na kukunjuka. Upungufu wa protini husababisha misuli kutofanya kazi yake kwa ufanisi hivyo mchezaji hukosa kasi anapokuwa uwanjani.

Pombe inachangia kushusha kiwango cha homoni ya kiume ijulikanayo kama Testosterone ambayo ndiyo inatuwezesha misuli kukua na kujikarabati, kwa mwanamichezo misuli imara ndio kila kitu.

Nihitimishe kwa kushauri wanamichezo kutokunywa pombe huku wanashiriki michezo, wakishindwa kuacha basi wanywe kwa kiasi. Lengo ni kulinda kiwango chao kisiporomoke na utimamu wa miili yao.