Straika aliyepigana na shabiki afungiwa
Muktasari:
- Kwa mujibu wa taarifa kutoka ZBL, Pina alipigana na shabiki katika mechi ya Ligi Kuu Zanzibar wakati Muembe Makumbi ikipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Mlandege kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja, Aprili 18, 2026.
KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Zanzibar (ZLB), imemfungia kucheza mechi tatu mfululizo mshambuliaji wa Muembe Makumbi, Abdalla Iddi ‘Pina’ kwa kosa la utovu wa nidhamu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ZBL, Pina alipigana na shabiki katika mechi ya Ligi Kuu Zanzibar wakati Muembe Makumbi ikipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Mlaadege kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja, Aprili 18, 2026.
Wakati huohuo, shabiki wa Mlandege, Fahad Mohammed ‘Mbaba’ ambaye alipigana na Pina, amefungiwa kuhudhuria uwanjani na kutizama mechi zote zitakazoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Adhabu hizo zimetolewa chini ya sura ya 20 (3) ya kanuni ya mashindano ya Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2025-2026.
Wakati huohuo, mchezaji wa Muembe Makumbi, Suleiman Hemed Khamis, amefungiwa michezo mitatu mfululizo ya ligi kwa kosa la utovu wa nidhamu kwa kutoka uwanjani na kupigana na mashabiki jukwaani katika mchezo dhidi ya KVZ uliochezwa Mei 3, 2026 kwenye Uwanja wa Mao.
“Timu ya Muembe Makumbi imetozwa faini ya Sh5 milioni kwa kosa la wapenzi wake kushindwa kutii masharti ya mdhamini mkuu mwenye haki ya matangazo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Pia, Meneja wa Muembe Makumbi City, Othman Othman (Mani) amefungiwa kuhudhuria kwenye mchezo wowote unaondaliwa na ZFF kwa siku 21 kwa kosa la kutoa lugha za matusi dhidi ya wasimamizi wa mchezo.
Mbali na hilo, mashabiki watatu wa Muembe Makumbi City, Hassan Fadhil ‘Bei’, Moh’d Fadhil ‘Kisube’ na Hashim Abdalla ‘Kibata’ wamefungiwa mwaka mmoja kuingia kuangalia michezo inayoandaliwa na ZFF kutokana na kile kilichoelezwa ni kosa la kukithiri kwao kutoa lugha za matusi wakati wa mchezo.
Matokeo ya mchezo baina ya Polisi dhidi ya KMKM, mechi iliyopangwa kuchezwa Mei 4, 2026 kwenye Uwanja wa Mao B, yamefutwa na timu ya Polisi FC imepewa alama tatu na mabao mawili.
“Timu ya KMKM SC imetozwa faini ya Sh3 milioni kwa kosa la kushindwa kufika uwanjani na wachezaji wanaostahiki kucheza kwenye mchezo huo, kwa mujibu wa Sheria 17 za Mpira wa Miguu, Sheria nambari 3.1 na kanuni ya Mashindano 2025/2026, SURA ya 21 (3) na kusababisha mchezo huo kuvunjika. Adhabu hizi ni kwa mujibu wa SURA ya 21(6) ya kanuni ya mashindano 2025/2026. Adhabu hizi zinaanza kutekelezwa kuanzia tarehe ya taarifa hii,” ilisema taarifa hiyo ya ZBL iliyotolewa Mei 7, 2026 na Ofisa Habari, Issa Chiwile.