Tabora United kuja kivingine Ligi Kuu

Muktasari:
- Timu hiyo imebakisha mechi mbili kufunga msimu huu ambapo Juni 18 itakuwa ugenini kucheza dhidi ya Azam huku ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mabao 2-1 mara ya mwisho Desemba 13, 2024.
KIKOSI cha Tabora United kimeingia kambini kujiwinda na mechi mbili za Ligi Kuu Bara zilizosalia kumalizia msimu huu, huku kocha mkuu Simonda Kaunda akieleza kuwa hali ya timu na wachezaji wako fiti.
Timu hiyo imebakisha mechi mbili kufunga msimu huu ambapo Juni 18 itakuwa ugenini kucheza dhidi ya Azam huku ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mabao 2-1 mara ya mwisho Desemba 13, 2024.
Baada ya hapo, Tabora itafunga msimu kwa kucheza na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Juni 22, huku timu hizo zikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 zilipokutana Desemba 17, 2024.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kaunda raia wa Zambia, alisema wachezaji wote wamerejea wakiwa katika hali nzuri ya utimamu wa kimwili isipokuwa beki wa kati Mkongomani Andy Bikoko anayetarajiwa kuwasili kuanzia leo.
“Wachezaji wote wako katika morali nzuri baada ya mapumziko mafupi. Kwa mazoezi ya siku hizi mbili tumemkosa Andy Bikoko ambaye tunafahamu alienda kwao DR Congo kwa ajili ya kumzika mama yake mzazi,” alisema Simonda.
Kocha huyo alisema kitendo cha kutopata matokeo mazuri katika mechi za karibuni kilichangia kushusha morali ya wachezaji, ingawa sasa maendeleo ni mazuri na wapo tayari kumalizia kwa heshima.
Kichapo cha bao 1-0 ilichokipata timu hiyo dhidi ya KMC, Mei 14, 2025, kimeifanya kufikisha mechi sita mfululizo za ligi bila ya ushindi tangu kilipoifunga Dodoma Jiji 1-0, nyumbani, Februari 28, 2025.
Simonda alitua, Aprili 18, 2025, akichukua nafasi ya Mzimbabwe Genesis ‘Kaka’ Mangombe aliyeondoka kutokana na mwenendo mbaya huku akiiongoza mechi nne za mashindano akipoteza zote.