Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tuisila, winga teleza mtesaji mabeki

WAKATI wa ujio wake nchini, mashabiki wa Yanga walisahau shughuli zao na kujitokeza kwa wingi kumpokea kutoka kwao DR Congo naye hakuwaangusha kwa kuanza mambo kwenye Kilele cha Siku ya Wananchi, Agosti 30.

Katika mchezo wa kirafiki wa kuhitimisha kilele cha siku hiyo, Tuisila Kisinda alifunga bao kali dakika ya 38 akipokea pasi murua ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ na kuukwamisha kwenye wavu wa timu ya Aigle Noir ya Burundi iliyoalikwa kuinogesha tamasha hilo.

Baada ya mchezo huo kumalizika miongoni mwa majina ambayo yalikuwa yakitajwa ni Tuisila kutokana na umahiri wake aliouonyesha alipokuwa na mpira mguuni na kuwasumbua mabeki wa Aigle Noir waliopewa kazi ya kumzuia.

Haikuchukua muda mrefu kwa Tuisila kujitambulisha mbele ya mashabiki wa Yanga kuwa moja ya nyota mwenye uwezo na anaweza kuisaidia timu hiyo katika safari yake ya kuwania ubingwa msimu huu.


BAO LA MUKOKO

Yanga ikiwa chini ya Kocha Zlatko Krmpotic walicheza mechi ya kwanza ugenini dhidi Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba na kushinda bao 1-0, lililofungwa na kiungo mkabaji Mukoko Tonombe. Bao hilo lililofungwa dakika 71,


lilitokana na umahiri wa Tuisila kuwapiga chenga mabeki wa Kagera Sugar akiwemo, David Luhende na kutoa pasi kwa mfungaji.


PENALTI SIMBA

Ubora huo wa kukimbia aliokuwa nao Tuisila alikuwa faida kwa Yanga walipokutana na Simba katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi dakika 28, aliutanguliza mpira mrefu na kumzidi beki wa kati Joash Onyango na mwamuzi kuamuru adhabu ya mkwaju wa penalti.

Tusila alisababisha penalti iliyopigwa dakika 31 na Sarpong. Mbali na kuisababisha penalti hiyo iliyotanguliza Yanga, lakini Onyango huenda itamchukua muda mrefu kumsahau Kisinda kwa namna alivyomtesa kwenye mchezo huo wa watani uliopigwa Novemba 7 na kumalizika kwa sare ya 1-1, Onyango akichomoa jioni kusawazisha makosa yake.

Katika mchezo huo Tuisila alikuwa akiwaburuza mabeki wa Simba atakavyo kama ambavyo amekuwa akifanya kwenye mechi nyingine zilizofuata ikiwamo ya Ruvu Shooting ambao mabeki wake waliamua kutumia nguvu kubwa kumzuia katika mechi waliyokufa kwa mabao 2-1.


UBORA

Licha ya kwamba Tuisila sio wa kumtegemea kukufungia mabao, lakini uwepo wake uwanjani na hasa usumbufu wa kasi yake na kuwaburuza mabeki, imekuwa msaada kwa timu yake.

Ubora alionao winga huyu kwanza ni mzuri katika kukimbia, kwani ana kasi kubwa, pia sio muoga na kama akicheza na beki lainilaini katika kuzuia wachezaji wa namna hiyo kila muda atakuwa anasoma jina na jezi namba ya Tuisila ama kumchezea madhambi yatakayomtia hasara. Kukimbia kwake kwa kasi kunamsaidia kupata nafasi za kupiga krosi na pasi kwa washambuliaji, kuanzisha mashambulizi ya hatari, kusababisha faulo na kona ambazo zinakuwa faida kwa Yanga, anapokuwa na mpira mguuni anavitu vingi kwani muda mwingine hupiga chenga za maudhi.

Licha ya ubora wake, lakini Tuisila ana mapungufu yake ikiwamo kuweza kuwapiga chenga mabeki na akapata nafasi ya kupiga krosi au pasi kwa mwenzake, lakini akachelewa kufanya maamuzi hadi kupoteza mpira. Ni kama anapenda kucheza jukwaa, lakini pia sio mzuri wa kukaba pindi timu inaposhambuliwa mara kwa mara.


LUNYAMILA AMCHAMBUA

Nyota wa zamani wa kimataifa, Edibily Lunyamila anasema Tuisila kiujumla ni mchezaji mzuri anaweza kukimbia katika nafasi anapokuwa hana mpira na kutengeneza mwanya wa mchezaji mwenzake kumpa pasi.

Pia anasema Tuisila mara baada ya kupokea mpira anagusa mara chache - muda muda mwingi anafikiria kukimbia kwenda langoni mwa timu pinzani kutengeneza shambulizi hatari na amefanya hilo katika mechi ya Kagera Sugar na Simba.

“Unajua tangu miaka ya nyuma silaha ya Yanga ni kuwa na mawinga wazuri kama huyu Tuisila, nadhani wamepata mchezaji anayestahili kucheza katika nafasi hiyo, ingawa bado ana upungufu wa kupoteza pasi na krosi pindi anapofika kwa walengwa,” anasema winga huyo aliyewika Biashara Shinyanga, Yanga, Simba, Malindi na Taifa Stars.


Imeandikwa na THOBIAS SEBASTIAN