Wadau wataka watoto wa kike wasitengwe mpira wa miguu

Muktasari:
- Wazazi wameomba kuwapa fursa watoto wa kikike kushiriki michezo hasa mpira wa miguu.
Baadhi ya wadau wa mpira wa miguu mkoani Lindi, wamewataka wazazi wawape fursa watoto wa kike kushiriki michezo hasa mpira wa miguu.
Wadau wa michezo mkoa wa Lindi wameyasema hayo leo kwenye kikao cha Samia Brazuka Cup kilichoshirikisha viongozi wa michezo wa ngazi za wilaya na mkoa kilichoandaliwa na Brazuka Football Club.
Mashindano hayo ya Brazuka Samia Cup yanaanzia mkoa wa Lindi, lakini lengo ni kuifikia mikoa 15 na kila mkoa watachagua wachezaji 33 watakaopata nafasi ya kwenda Afrika Kusini katika majaribio.
Dickson Maluchila, Mwenyekiti wa Chama cha Soka wilayani Lindi, amewaomba wazazi kuwaruhusu watoto wa kike kushiriki mashindano ya Brazuka Samia cup.

"Wazazi wetu niwaombe wawape watoto wa kike nafasi ya kushiriki michezo hasa mpira wa miguu hii ni fursa kwa sababu mchezo huu sio wa watoto wa kiume tu. Lengo letu kama wilaya na mkoa ni kukuza vipaji vya vijana wetu hivyo, ujio wa brazuka utatusaidia kuinua vipaji vya vijana wetu," amesema Maluchila.
Jamali Lisuma, Ofisa Michezo Manispaa ya Lindi, amesema ujio wa brazuka kwao ni mafanikio kwa sababu wao wanatekeleza mipango walio ikusudia, wana vituo Mpilipili, Mnazi Mmoja, Kiwalala na maeneo mengine hivyo ujio wa mashindano hayo utaenda kuongeza nguvu na wameyapokea kwa mikono miwili.
Katibu wa Chama cha Soka wilayani Kilwa, Akida Hassan amesema wilayani humo kuna vijana wengi wana vipaji ila hawapati nafasi ya kuonekana.
"Ujio wa mashindano haya ya Brazuka Samia Cup utatusaidia sana kwa sababu tunawatafuta watu kama hao. Kilwa tuna vipaji vingi sana, wale ambao hawakupata nafasi yakuonekana wataenda kuonekana kupitia mashindano haya wakiwa huko huko wilayani," amesema Akida.
Lilian Kitunga ambaye ni Mratibu wa Brazuka amesema mashindano hayo yatajumuisha na watoto wa kike.
"Vijana wako wengi sana wana changamoto ya maisha duni, hivyo mashindano haya na wasichana tunawahitaji sana wapo ambao wapo nje ya shule, lakini tunaomba na sisi watoto wa kike mkatuinue, japo kuna rushwa ya ngono nalo hili mkaliangalie," amesema Kitunga.
Naye Mkurungezi wa Brazuka, Mchatta Erick amesema suala la kuinua mchezo wa mpira wa miguu tusiiyachie TFF ama serikali peke yako ni jambo la wadau wote wa mpira wa miguu.
"Tutafanya mashindano haya katika mikoa 15, lakini tumeamua kuanza na mkoa wa Lindi halafu tutaendelea mikoa mingine. Tusiilaumu TFF wala serikali swala la mpira ni la kwetu sote. Tumeenda Afcon mara 3, lakini hatusongi mbele tunaishia hatua hiyo hiyo ya makundi hivyo hivi vitu vinahitaji maandalizi tunatakiwa tuanze chini kabisa," amesema Mchatta.
Mchatta ameongeza kwa kusema; "Changamoto ya mpira wa miguu sio ya mtu mmoja ni jambo la wadau wote. Kuna vijana wengi wanavipaji lakini wanaishia kuwa bodaboda, wavuvi wauza mitumba na vipaji vyao vina potea. Katika mashindano haya timu zitatokea chini chini kabisa. Pia malengo yetu ni kukuza utalii katika mkoa wa Lindi," amesema Mchatta.
Kwa upande wa mgeni rasmi ambaye ni Ofisa Elimu, Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi, Philip Siaya amesema vijijini kuna vipaji vingi, lakini havipati nafasi ya kuonekana kwa sababu hawajapata fursa yakuonekana.
"Vijijini kuna vipaji vingi sana, lakini havionekani kwa sababu havijapata fursa, hivyo nimefurahi Brazuka kuja mkoani kwetu kutafuta vipaji na watavipataje ni kwa kuanzisha Brazuka Samia Cup, hivyo viongozi tuliopo hapa ni wawakilishi wa watu wote wa mkoa wa Lindi," amesema Siaya.