Watatu wapya watua Yanga

KUNA watu watatu muhimu katika benchi la ufundi la Yanga hawatakuwepo kwa msimu ujao na wote ni raia wa kigeni, lakini Kocha Nabi kibabe amewashusha mafundi wengine akitumia fedha za bilionea wa GSM kuwapokonya Waarabu wa Tunisia watu hao wa kazi.
Yanga haitakuwa na kocha msaidizi, Sighr Hamad lakini pia mtaalamu wa mazoezi ya viungo Jawad Sabri na daktari Msauzi wa viungo Fareed Cassem ambao kwa sababu mbalimbali za kupata kazi mpya hawatakuwa sehemu ya timu hiyo kwa msimu ujao.
Tayari fasta Nabi ameliambia Mwanaspoti kwamba kuna mtu amemchomoa katika klabu ya Esperance ya kwao Tunisia na wakati wowote atatua ndani ya kambi yao kuanza kazi haraka akimsifia tajiri wa GSM, Gharib Mohamed kumaliza mchakato wa kumnunua haraka.
“Kuna mtu namleta kutoka Tunisia toka klabu ya Esperance ni kocha mzuri sana atakuja hapa haraka wakati wowote kuanzia leo (jana mchana) kuja kuanza kazi, huyu ni kocha mzuri sana nampongeza Gharib kwa kusimamia vyema kumleta,” alisema kocha huyo.
Nabi alisema mtu wa pili ambaye ni mtaalamu wa mazoezi ya viungo naye ataungana na timu hiyo haraka wakati wowote kuanzia leo kuja kuendeleza pale alipoishia Jawad ambaye tayari alishaanza kukubalika kwa mazoezi yake kikosini.
Mtaalamu wa tatu kati ya hao ni daktari wa viungo tayari ameshatua kambini akitambulika kwa jina la Youssef Ammar ambaye tayari ameshaanza kazi rasmi ndani ya timu hiyo akichukua nafasi ya Cassem ambaye ameshaachana na Yanga.
SOMA HAPA:Yanga yataka kutesti na Simba Morocco
“Tumewapata watu wazuri ambao watakuja kuendelea kujumuika na sisi wengine katika kutekeleza majukumu yetu ya kujenga timu naamini wataisaidia sana timu,” alisema Nabi.