Wawakilishi wataka ZFF kupata gawio TFF
Muktasari:
- Naibu Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo Zanzibar, Ali Abdulgulam Hussein amesema wizara hiyo imejiridhisha ZFF haina sheria inayoelekeza kudai mgao wa fedha au chochote kutoka TFF, wala TFF haina kifungu cha kutoa mgao kwenda ZFF.
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wamehoji kuhusu Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) kupata gawio la fedha kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo Zanzibar, Ali Abdulgulam Hussein amesema wizara hiyo imejiridhisha ZFF haina sheria inayoelekeza kudai mgao wa fedha au chochote kutoka TFF, wala TFF haina kifungu cha kutoa mgao kwenda ZFF.
Naibu huyo ametoa kauli hiyo kwa niaba ya Waziri Rikizi Pembe Juma wakati akijibu swali lililoulizwa na Mwakilishi, Mahmoud Shineni Ali aliyetaka kujua juu ya ZFF kupata gawio kutoka TFF, FIFA na CAF.
Akitoa ufafanuzi wa hilo, amesema kwa sasa wizara imejielekeza zaidi juu ya wazo la kuiwezesha ZFF kujitegemea na kupata ufumbuzi wa uanachama wa FIFA au CAF.
"Wizara imejiridhisha ZFF haina sheria inayoelekeza kudai mgao wa fedha au chochote kutoka TFF, wala TFF haina kifungu cha kutoa mgao kwa ZFF," amesema.
Amesema Serikali ina uhakika endapo ZFF litapata uanachama halali wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), fedha na ruzuku zitakazotolewa na mashirikisho hayo zitaelekezwa moja kwa moja ZFF bila kupitia TFF na ZFF haina ruzuku kisheria inayotakiwa kupata kutoka TFF.
Pia, amesema Serikali ina msimamo thabiti ZFF haipaswi kupata haki zake kutoka TFF, ila haki yake ipo kutoka FIFA na CAF kama itapata uanachama.