Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanayosubiriwa uzinduzi uwanja wa Singida

SINGIDA Pict
SINGIDA Pict

Muktasari:

  • Uwanja huo uliopo Mtipa mkoani Singida, umejengwa kwa viwango vya kisasa ukiwa na nyasi bandia kwa kushirikiana na wadhamini wakuu wakiwamo Airtel, Azam, GSM, NBC, SBS, na MO Dewji. Uwanja huu una uwezo wa kuchukua mashabiki 5,000 hadi 7,000 na unatarajiwa kuwa kitovu cha mashindano makubwa ya kitaifa na kimataifa.

LEO Jumatatu, Machi 24, 2025, ni siku ya kihistoria kwa wapenda soka wa Mkoa wa Singida na taifa kwa ujumla, kwani klabu ya Singida Black Stars inazindua rasmi uwanja wake mpya. Uzinduzi huu ni hatua kubwa kwa klabu hiyo, ambayo imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo ili kuinua kiwango cha soka nchini.

Uwanja huo uliopo Mtipa mkoani Singida, umejengwa kwa viwango vya kisasa ukiwa na nyasi bandia kwa kushirikiana na wadhamini wakuu wakiwamo Airtel, Azam, GSM, NBC, SBS, na MO Dewji. Uwanja huu una uwezo wa kuchukua mashabiki 5,000 hadi 7,000 na unatarajiwa kuwa kitovu cha mashindano makubwa ya kitaifa na kimataifa.

Sherehe za uzinduzi zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na michezo, huku mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA. Aidha, viongozi wa TFF nao wanatarajiwa kushiriki.

Burudani mbalimbali zimetayarishwa kabla ya mechi kuu, ikiwa ni pamoja na muziki kutoka kwa wasanii maarufu wa Bongo Fleva, michezo ya asili, na maonesho ya utamaduni wa Kisingida. Mashabiki watapata fursa ya kushuhudia historia ikiandikwa kwa mara ya kwanza kwenye uwanja huu mpya.

Kilele cha tukio hili kitakuwa ni mchezo wa kirafiki kati ya wenyeji Singida Black Stars na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC utakaochezwa kuanzia saa 10 jioni. Mechi hii inatajwa kuwa ya kuvutia kutokana na nafasi za timu hizi katika msimamo wa ligi, ambapo Yanga wanaongoza kwa pointi 58 huku Singida Black Stars wakiwa nafasi ya nne na pointi 44.

Licha ya kuwa mechi ya kirafiki, upinzani baina ya timu hizi mbili umeibua hamasa kubwa kwa mashabiki. Singida Black Stars wanataka kutumia uwanja wao mpya kuonyesha ubabe wao, huku Yanga wakitaka kuendeleza rekodi yao nzuri dhidi ya wapinzani wao.

Hata hivyo, mechi hii inachezwa kipindi ambacho baadhi ya wachezaji wapo katika majukumu ya timu zao za taifa kwa mujibu wa kalenda ya FIFA. Hii inamaanisha kuwa vikosi vya pande zote viwili vitakuwa na mabadiliko, jambo linaloweza kuleta mtazamo mpya wa kiufundi kwa benchi za ufundi.

Kocha wa Singida Black Stars, David Ouma alisema licha ya kukosa baadhi ya nyota wake wa kikosi cha kwanza, amewaandaa wachezaji wake kikamilifu kwa mchezo huu.

“Huu ni uwanja wetu mpya, tunataka kuuanza kwa ushindi ili kutoa heshima kwa mashabiki wetu na wadhamini waliotuunga mkono,” alisema.

Kwa upande wa Yanga SC, Miloud Hamdi alisema huu ni mchezo wa maandalizi kuelekea hatua ya mwisho ya ligi, lakini pia ni fursa kwa wachezaji wengine kuonyesha uwezo wao.

“Hatutaki kupoteza mchezo huu hata kama ni wa kirafiki. Tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema.

Wachezaji wa Singida Black Stars wanaotegemewa kung’ara kwenye mchezo huu ni pamoja na mshambuliaji wao hatari, Jonathan Sowah ambaye ameonyesha kiwango bora katika michezo ya hivi karibuni kwa kufunga mabao saba katika mechi 7.

Kwa upande wa Yanga SC, pamoja na baadhi ya nyota wao kuwa na majukumu ya timu za taifa, bado wana kikosi imara chenye uwezo wa kupata matokeo chanya.

Mashabiki wa Singida Black Stars wamehamasika kwa kiasi tangu juzi Jumamosi na wanatarajiwa kufika kwa wingi kushuhudia tukio hili la kihistoria. Baadhi yao wameeleza kuwa hii ni hatua kubwa kwa klabu yao na kwamba wana matumaini kuwa uwanja huu utaleta mafanikio zaidi kwa timu yao.