Yanga Kigelegele aishiwa pozi

SHABIKI wa Yanga, maarufu kama Yanga Kigelegele, baada ya matokeo ya 1-1 ya timu yake dhidi dhidi ya Polisi Tanzania jana Jumapili ya Machi 7, 2021 ameishia kusema anaipenda timu hiyo ' I love Yanga' na kushindwa kupiga kigelegele, kama kawaida yake.
Matokeo hayo amekiri yamemuumiza na amewaomba viongozi kuitengeneza timu itakayoendana na shamlashamla zao zenye matumaini makubwa ya kunyakua taji la ubingwa kwa msimu huu.
"Sina maana kwamba sare saba tulizopata na kufungwa mchezo mmoja ndio mwisho wa safari yetu ya imani kwamba Yanga inachukua ubingwa msimu huu, lakini tunaomba kufanyike kitu cha ziada ambacho kitakuwa kinatupa matumaini," amesema na ameongeza kuwa,
"Tumetoka mbali kuja Arusha kuishangilia timu, kumbuka tulianzia Tanga ambako timu ilipoteza mechi dhidi ya Coastal Union, lakini tukajipa moyo kwamba mchezo na Polisi Tanzania tutashinda lakini mwisho wa siku tunaambulia sare, inaumiza sana," amesema.
Amesema bado anaamini timu yake ina nafasi ya ubingwa na ametaja silaha kubwa ya kufikia ndoto zao kwamba ni kushikamana kupigania malengo yatimie.
"Tuanzie tulipoishia, nawaomba mashabiki wenzangu tusiache kwenda uwanjani kuishangilia timu, tukiacha tunakuwa tunawapa nguvu wapinzani wetu kwamba tumenyenyua mikono juu ya kushindwa, bado Yanga ina nafasi ya ubingwa, ili mladi mechi bado zipo," amesema.