Yanga, Tz Prisons mambo magumu Sumbawanga

DAKIKA 45 za kipindi cha kwanza, hazikuwa rahisi kwa mastaa wa Yanga na wenyeji wao Tanzania Prisons, kutokana na Uwanja wa Nelson Mandela kuwa na maji, hivyo walijikuta wakibutuabutua mipira.
Mpira ulianza kwa ugumu, huku wachezaji wa timu zote mbili wakijaribu kupeleka mipira mbele, kuna wakati pasi zilikuwa zinakataa kwenda na mpira kutwama kwenye maji.
Angalau mashuti ya mbali ndio yalikuwa na uhai wa kwenda kulenga kwenye malengo ya makipa wao kwa maana ya Metacha Mnata upande wa Yanga na Jeremiah Kusubi kwa upande wa Prisons.

Dakika ya 30 beki namba tatu wa Prisons, Benjamini Asukile alijaribu kupiga shuti la mbali ambalo vipimo vyake vilikosea kidogo tu, kulenga lango la Yanga.
Kwa upande wa Yanga, winga wao Mkongomani Tuisila Kisinda licha ya uwanja kuwa na maji,haukumzuia kukimbia mbio akitokea pembeni na dakika ya 41 usingekuwa umakini wa kipa wa Prisons, angeipatia timu yake bao.
Kipa wa Prisons aliongeza umakini wa kumsoma Kisinda baada ya kuona mabeki wake wa pembeni wamezidiwa mbio, hivyo akaudaka mpira.
Mechi kutoka viwanja vingine, Polisi na Azam FC wametoshana nguvu kwa kutoka suluhu dakika 45 za kipindi cha kwanza na wageni wao Azakm, huku Namungo ikiongoza kwa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, bao lililofungwa na Idd Kipagwile dakika ya 10.