Yanga yaisubiri Simba, Mlandege fainali Muungano Cup
Muktasari:
- Hiyo ilitokana na bao lake la kwanza kufungwa dakika ya tano tu, mfungaji akiwa mshambuliaji Prince Dube akimalizia vizuri asisti ya kiungo, Allan Okello.
BINGWA mtetezi wa Kombe la Muungano, Yanga imefanikiwa kurudi kwenye fainali ya michuano hiyo baada ya kuichapa Azam FC kwa mabao 2-1, huku sasa ikiisubiri Simba au Mlandege.
Kwenye mchezo huo wa nusu fainali uliopigwa leo Aprili 25, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Yanga ikianza kwa kasi, ikatengeneza ushindi wake ndani ya dakika 25 za kwanza.
Hiyo ilitokana na bao lake la kwanza kufungwa dakika ya tano tu, mfungaji akiwa mshambuliaji Prince Dube akimalizia vizuri asisti ya kiungo, Allan Okello.
Azam ikafanya shambulizi zuri dakika 24, lakini beki, Fuentes Mendoza akashindwa kumalizia shuti lake likitoka nje kidogo.
Wakati Azam ikitafuta bao la kusawazisha, ikajikuta inaruhusu la pili dakika ya 25, Yanga ikifanya shambulizi la haraka mfungaji akiwa kiungo Maxi Nzengeli akimalizia asisti ya Dube.
Azam haikukata tamaa, ikaendelea kujipanga dakika ya 40 ikapata nafasi nyingine nzuri, kichwa cha beki na nahodha wake, Lusajo Mwaikenda lakini kikatoka nje kidogo juu, timu hizo zikienda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili, Azam ikianza na mabadiliko ya eneo la kiungo ikimtoa James Akaminko nafasi yake ikichukuliwa na Sadio Kanoute, ikafanikiwa kurudisha utulivu na kuirudisha nyuma Yanga.
Dakika ya 77, Azam ikafanikiwa kupata bao kupitia kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' kwa shuti akiunasa mpira ulioshindwa kuokolewa na mabeki wa Yanga.
Ushindi huo unaipeleka Yanga fainali ya pili mfululizo katika michuano hiyo ikimsubiri mshindi wa mchezo wa nusu fainali ya pili itakayopigwa kesho Jumapili kati ya Mafunzo dhidi ya Simba.
Fainali ya michuano hiyo itachezwa Aprili 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, ambapo Yanga inatetea taji lake hilo ililolichukua mwaka jana kwa kuifunga JKU bao 1-0.