Prime
Yanga yamrudisha beki kutoka Uganda
![Beki Pict](/resource/blob/4924514/19e3c275b6586398b577b38633c1ad13/beki-pict-data.jpg)
Muktasari:
- Inaelezwa Yanga iliyo chini ya kocha Miloud Hamdi inataka kumrejesha aliyekuwa beki wa kati wa timu ya vijana U-20, Shaibu Mtita anayekipiga Wakiso Giants ya Uganda kwa mkopo.
KIKOSI cha Yanga kesho jioni kitashuka Uwanja wa KMC Complex katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, lakini kabla ya kipute hicho kupigwa inaelezwa benchi la ufundi la timu hiyo lipo mbioni kumrejesha aliyekuwa beki aliyekuwa Uganda.
Inaelezwa Yanga iliyo chini ya kocha Miloud Hamdi inataka kumrejesha aliyekuwa beki wa kati wa timu ya vijana U-20, Shaibu Mtita anayekipiga Wakiso Giants ya Uganda kwa mkopo.
Ishu hiyo inakuja baada ya Yanga kuhusishwa na tetesi za kumtaka Lameck Lawi wa Coastal Union aliyekuwa anawaniwa na vigogo Simba na Yanga.
Kwa sasa Yanga ina mabeki wa kati watatu, Dickson Job, Ibrahim Abdullah 'Bacca' na Bakari Mwamnyeto ambaye amekuwa akikosa nafasi mbele ya wenzake.
Tangu dirisha dogo Yanga imekuwa ikipambana kupata beki wa kati mwingine atakayesaidiana na nahodha Mwamnyeto aliyekosa mechi kadhaa baada ya pacha ya Job na Bacca kuwa bora.
Hata hivyo, inaelezwa kocha Hamdi baada ya kuletewa video za beki huyo anayekipiga Uganda akaagiza kuletewa ili kuja kuongezea nguvu eneo hilo.
Mmoja wa benchi la ufundi la timu ya vijana ya Yanga aliliambia Mwanaspoti kuwa msimu ujao atarejeshwa kikosini baada ya kupata uzoefu wa Ligi ya Uganda.
"Ni kweli yupo kwenye mipango ya msimu ujao wa timu, awali alikuja wakati ambao mabeki wote wako vizuri na hakukuwa na changamoto yoyote hivyo ikashauriwa atolewe kwa mkopo ndio ikatokea ofa ya Wakiso," alisema na kuongeza.
"Kutokana na anachokifanya huko pia tunamfuatilia, viongozi wameona ni bora arudi kuliko kutafuta wengine na isitoshe anacheza na anapata nafasi ambayo imemuongezea kujiamini zaidi."
Beki huyo ambaye alipandishwa na Yanga wakati wa kocha Miguel Gamondi akicheza mechi kadhaa za Mapinduzi Cup na Kombe la FA, kwa sasa ndio beki tegemeo.
Licha ya Wakiso Uganda inayoshiriki Ligi Kuu kuwa nafasi ya 14 kati ya 16 kwenye msimamo wa ligi hiyo na pointi 13, nyota huyo ameonyesha kiwango bora na kuchukua namba kikosi cha kwanza.
MECHI ZAKE
Hadi sasa imefikia raundi ya 16 ya ligi huku Mtita akicheza mechi 14 kwa dakika 1031 akiruhusu mabao 23.
Mechi yake ya kwanza akiwa na uzi wa Wakiso Giants, Septemba 15 dhidi ya Bright Stars zilipotoka sare ya 1-1 na kitasa hicho kikimaliza dakika 90.
Maroons 2-3 akimaliza dakika 90, Mbale Heroes 0-1 (83), UPDF 1-0 (90), Vipers 2-0 (90), Express 0-0 (15), Lugazi 0-0 (7), Villa 6-1 (26), URA SC 3-0 (90), Police 2-1 (90), Mbarara City 0-0 (90), Kitara 0-0 (90), BUL 1-1 na Villa 1-1 akimaliza dakika (90).