Yanga yataka kutesti na Simba Morocco

YANGA wameanza jeuri. Wakati wanatua jana nchini Morocco, mkuu wa msafara wao akatoa kauli moja ya kichokozi kwa kujiamini huku viongozi wenzie wakimsapoti.
Wanataka kama vipi watesti mitambo kwa kucheza mechi ya kirafiki na Simba iliyopo kambini mjini Rabat. Kutoka Casablanca walipofikia Yanga na Rabat walipo Simba ni mwendo wa saa moja na dakika zisizozidi 20 kwa gari.
Sasa mkuu wa msafara wa Yanga ni makamu mwenyekiti wa timu hiyo, Frederick Mwakalebela ameliambia Mwanaspoti kwamba wao wamemaliza usajili na wanajipanga kwa michuano ya kimataifa.
Mwakalebela ambaye ni kiongozi wa zamani wa TFF, alisema usajili walioufanya ni wa viwango na kazi iliyobaki ni kocha wao Nesreddine Nabi kuingiza ufundi wake, na baada ya hapo wako tayari hata kukutana na Simba hukuhuku kabla hawajageuka kurudi Tanzania.
Alisema Yanga itakuwa tayari wakikutana na watani wao hukuhuku Morocco wote wakiwa katika maandalizi kabla hata ya Septemba 25 ya mchezo wa ngao ya hisani. “Sisi tumemaliza usajili na sasa timu imekamilika, hatudhani kama tutakuwa na ulazima sana wa kufanya usajili labda itokee kocha ahitaji kitu cha ziada, tunaamini watu tulioleta sasa watairudisha heshima ya makombe ya hii timu.
“Tunaposema tumeenea watu wasidhani tunatania na tutaongea na kocha kama atakubali, basi hawa jamaa zetu tukutane nao kwanza hukuhuku Morocco kabla hatujarudi nyumbani na bahati nzuri kama watakubali tunaamini huku wenzetu wa hapa wana waamuzi bora kabisa ambao watatoa haki katika mechi hii.
“Tunajua tutakutana nao Septemba 25, lakini kama wataona inafaa basi tujaribu silaha zetu hukuhuku ili kila mmoja ajue amesajili kipi kuelekea msimu ujao kisha tukikutana tena kwenye ngao kusiwe na lawama,” alisisitiza kiongozi huyo na kuwahakikishia wana Yanga kwamba msimu huu mambo yatakuwa moto.
Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika imepangwa kuanza na River United ya Nigeria, Septemba 10 kwenye Uwanja wa Mkapa na kurudiana wiki mbili baadaye ugenini.