Gor Mahia yatwaa ubingwa wa Ligi ya Kenya 2025-26
Muktasari:
- Kwa sasa Gor Mahia ipo kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 68 ikicheza mechi 32, huku AFC Leopards inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 64 ikibakiza mechi moja mkononi, hivyo hata ikishinda mchezo wa mwisho itafikisha pointi 67, moja nyuma ya Gor Mahia ilizonazo sasa.
TIMU ya Gor Mahia inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya, imetangazwa kuwa bingwa mpya wa ligi hiyo ikibakiza mechi mbili kumaliza msimu huu.
Kwa sasa Gor Mahia ipo kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 68 ikicheza mechi 32, huku AFC Leopards inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 64 ikibakiza mechi moja mkononi, hivyo hata ikishinda mchezo wa mwisho itafikisha pointi 67, moja nyuma ya Gor Mahia ilizonazo sasa.
Bidco United na Sofapaka zimeshashuka daraja kwani hata zikishinda mechi mbili walizobakiza hazitaweza kufikisha pointi 35 ilizonazo Ulinzi Stars iliyopo nafasi ya 16 katika mechi 32.
Bidco ipo nafasi ya 17 kwa pointi 23 ikibakiza mechi mbili, ikishinda mbili zijazo itafikisha pointi 29 wakati Sofapaka ipo mkiani kwa pointi 19 ikicheza mechi 32, ikishinda mechi zilizobaki itakuwa na pointi 25.
Huu ni ubingwa wa 22 katika historia ya Gor Mahia iliyoanzishwa mwaka 1968, mara ya mwisho ilichukua msimu wa 2023-2024. Pia ndio timu iliyobeba ubingwa mara nyingi kuliko timu yeyote ya Ligi Kuu Kenya huku watani zao AFC Leopards ikibeba mara 13.
Katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2019, Gormahia ilitawala ligi hiyo ikibeba mara sita katika misimu saba.
Ukiacha Ligi Kuu, pia Gor Mahia imetwaa ubingwa wa FA mara 10 sawa na AFC Leopards, Super Cup (4), pia CECAFA (3) ikiwa ni idadi ndogo kwa watani zao AFC waliobeba mara tano ambayo ni mara nyingi zaidi kuliko timu yoyote ya Afrika Mashariki na Kati.