Kenya yakusanya Dola 316K mauzo ya wachezaji, Tanzania ikichangia Dola 9276
Muktasari:
- Ripoti hiyo ya Global Transfer 2024 ilitolewa wiki iliyopita imeonyesha jumla ya uhamisho wa wachezaji wa kiume duniani ulifikia kiwango cha juu cha 22,779 mwaka jana na gharama za uhamisho kufikia Dola 8.59 bilioni (KSh1.1 trilioni).
Ripoti ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) imeiorodhesha Kenya miongoni mwa nchi zilizovuna pesa kutokana na mauzo ya wachezaji wa kiume nje ya nchi, ikikusanya Dola 316,000 (Ksh 40.8 milioni) mwaka jana.
Ripoti hiyo ya Global Transfer 2024 ilitolewa wiki iliyopita imeonyesha jumla ya uhamisho wa wachezaji wa kiume duniani ulifikia kiwango cha juu cha 22,779 mwaka jana na gharama za uhamisho kufikia Dola 8.59 bilioni (KSh1.1 trilioni).
Ukanda wa Afrika Mashariki, imeonyesha Kenya inaifuata Tanzania kwa kiasi cha fedha ilichokusanya, Ksh40.8 milioni, ikilinganishwa na jirani zao iliyokusanya Dola 896,000 (Ksh115.7 milioni).
Ripoti hiyo imesema wachezaji 37 kutoka Ligi Kuu Kenya walihamia kwenye ligi za nje mwaka jana na kusababisha ongezeko la asilimia 76.2 katika ada za uhamisho, huku Tanzania ikipokea wachezaji 11 na Uganda saba.
Kwa mujibu wa ripoti, idadi kubwa imekimbilia Tanzania kutokana na ushindani wa ligi ya nchini humo Ligi Kuu ya Tanzania (TPL) na utawala wake na ndiyo inayofuatiliwa zaidi katika ukanda wa Cecafa.
Sababu nyingine ni wachezaji wa ligi hiyo (TPL) kupata nafasi kubwa ya kuonekana kwa mawakala wa wachezaji wa kimataifa kwani ligi hiyo hurushwa mubashara kwenye runinga.
Ripoti hiyo imeonyesha pia kwa dunia kwa jumla, England ndiyo inayoongoza kwa mauzo ya wachezaji nje ikikusanya Dola 1.34 bilioni (Ksh173 bilioni), huku Mali ikiongoza kwa Afrika na ilikusanya Dola 25.4 milioni (Ksh3.2 bilioni).
Ripoti hiyo ya nusu mwaka iliyotoka mwezi Septemba mwaka jana, ilionyesha uhamisho mkubwa wa wachezaji wa Kenya uliongozwa na kiungo Stanley Wilson (18) kutoka Kariobangi Sharks kwenda AIK Football, ukigharimu Ksh25.7 milioni, ukifuatiwa na wa kiungo Duke Abuya kutoka Kenya Police kwenda Young Africans Sports Club (Yanga) kwa mkopo uliogharimu Ksh6.5 milioni.
Uhamisho mwingini ni wa wachezaji kama mshambuliaji Eric Kapaito kutoka Tusker kwenda Namungo FC ya Tanzania, kipa Brian Bwire kutoka Tusker kwenda Polokwane City ya Afrika Kusini, na beki Christopher Oruchum kutoka Posta Rangers kwenda Pamba Jiji FC ya Tanzania. Kwa jumla klabu za Tanzania zililipa Ksh236.9 milioni.
Hata hivyo, ripoti hiyo, haikubainisha kiasi kilichotumika na klabu za Kenya kusajili nyota wa kigeni, licha ya kuwa FKF-PL ilirekodi uhamisho wa wachezaji 36 kutoka nje.
Uganda iliongoza kwa kuwa na wachezaji wengi kutoka ligi ya Kenya (8) huku Tanzania ilikuwa nao (6).
Kwa upande wa soka la wanawake wachezaji 21 kutoka Kenya walihamia nje ya nchi, na wachezaji wanne wa kigeni walijiunga na klabu za Kenya huku Tanzania ikichukua wachezaji 11 kutoka Kenya.