Mechi saba Ligi Kuu zamshtua Mkenya Mtibwa Sugar
Muktasari:
- Mara ya mwisho kwa timu hiyo kushinda mechi ya Ligi Kuu Bara ni ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons, Februari 2, 2026. Kuanzia hapo imeshachapwa nne na kutoka sare tatu kati ya saba.
BAADA ya Mtibwa Sugar kucheza mechi saba mfululizo za Ligi Kuu Bara bila ya ushindi, kocha wa timu hiyo, Mkenya Yusuf Chippo, amesema ana kazi kubwa ya kufanya kipindi hiki cha mapumziko, ili kurejesha upya morali ya kikosi hicho.
Mara ya mwisho kwa timu hiyo kushinda mechi ya Ligi Kuu Bara ni ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons, Februari 2, 2026. Kuanzia hapo imeshachapwa nne na kutoka sare tatu kati ya saba.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chippo amesema sababu ya mwenendo mbovu wa timu hiyo ni kushindwa kutumia vizuri nafasi za kufunga, japo eneo la kujilinda bado linafanya makosa ya mara kwa mara, jambo ambalo anaendelea kulifanya kazi haraka.
“Inapotokea hatujafunga bao basi na sisi tusiruhusu, ila imekuwa ni tofauti kwa mechi zetu zilizopita, nadhani ni upepo pia mbaya tunaokutana nao kwa sasa, kwa sababu hata mwanzoni tulifanya vizuri na wachezaji tulionao,” amesema.
Pia amesema licha ya nafasi ya tisa iliyopo, haiwapi uhakika wa kubaki Ligi Kuu msimu ujao kutokana na gepu la pointi lililopo kutoka kwa wapinzani wao, hivyo, wanapaswa kuongeza uangalifu.
“Unapozungumzia mechi saba maana yake unazungumzia pointi 21, ila kati ya hizo sisi tumepata tatu na kudondosha 18, ni jambo la hatari sana, lakini bado tuna nafasi ya kurekebisha hizo changamoto katika mechi 11 zilizobaki,” amesema Chippo.
Chippo aliyeachana na Murang’a SEAL ya kwao Kenya tangu Agosti 21, 2025, alijiunga na Mtibwa Novemba 17, 2025 akishirikiana na Kocha Msaidizi, Awadh Juma ‘Maniche’, aliyeipandisha timu hiyo Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025.
Mtibwa imecheza mechi 19 za Ligi Kuu, imeshinda tano, sare nane na kupoteza sita, ikiwa nafasi ya tisa na pointi 23