Mkenya kulamba dili jipya Pamba Jiji
Muktasari:
- Nyota huyo aliyesaini mkataba wa miaka miwili, amebakisha miezi sita baada ya msimu huu wa 2025-2026 kuisha, ingawa kwa sasa mabosi wa timu hiyo wameanza mazungumzo ya kuongeza mwingine, ikiwa ni pendekezo la Kocha Mkenya, Francis Baraza.
MABOSI wa Pamba Jiji wameanza mchakato wa kumuongezea mkataba mpya mshambuliaji wa kikosi hicho, Mkenya Mathew Momanyi Tegisi baada ya kuridhishwa na kiwango chake tangu amejiunga na timu hiyo.
Nyota huyo aliyesaini mkataba wa miaka miwili, amebakisha miezi sita baada ya msimu huu wa 2025-2026 kuisha, ingawa kwa sasa mabosi wa timu hiyo wameanza mazungumzo ya kuongeza mwingine, ikiwa ni pendekezo la Kocha Mkenya, Francis Baraza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji (CEO), Peter Juma Lehhet, amesema maboresho yatakayofanyika na timu hiyo yatazingatia matakwa ya benchi la ufundi la kikosi hicho, japo ni kweli taratibu hizo zimeshaanza mapema.
“Kuna wachezaji tunaendelea na mazungumzo nao kwa ajili ya kuongeza mkataba mpya na tutakapofikia muafaka tutaweka wazi juu ya hilo, kwa sasa malengo yetu ni kuhakikisha tunamaliza msimu vizuri kwa mechi zetu zilizobakia,” amesema Lehhet.
Momanyi aliyetokea Shabana ya Kenya, alijiunga na Pamba dirisha dogo la Januari 2025 na hadi mwisho wa msimu wa 2024-2025, alifunga mabao saba ya Ligi Kuu, akiwa ndiye aliyeongoza katika kikosi hicho.
Nyota huyo aliendeleza alipoishia akiwa na Shabana FC, kwa sababu kabla ya kujiunga na Pamba alikuwa pia amefunga mabao matano kwao Kenya, nyuma ya mshambuliaji mwingine wa kikosi hicho, Brian Michira aliyekuwa anaongoza kwa kufunga saba.
Msimu huu wa 2025-2026, tayari mshambuliaji huyo amefunga mabao matano ya Ligi Kuu Bara akiwa ndiye anayeongoza ndani ya kikosi hicho, huku bao lake la mwisho lilikuwa ni la ushindi wa 1-0 dhidi ya KMC, Mei 20, 2026.