Wiki tatu zampa Mkenya ahueni
Muktasari:
- Kocha huyo anakumbukwa na mashabiki hasa baada ya kukiongoza kikosi cha Ulinzi Stars kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu ya Kenya ‘KPL’ kati ya 2003 na 2005 na kuhudumu akiwa kocha msaidizi wa Harambee Stars kuanzia 2008 hadi 2011.
KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mkenya, Yusuf Chipo, amesema mapumziko ya wiki tatu kwa timu hiyo yamempa nafasi ya kufanyia kazi maeneo muhimu mawili ya kujilinda na ya ushambuliaji, ambayo yamekuwa ni changamoto kubwa kwenye mechi zilizopita.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chipo amesema mwenendo wa kikosi hicho katika mechi tatu zilizopita sio mzuri kutokana na makosa mbalimbali katika maeneo ya kujilinda na kushambulia, ambapo kwa sasa wanaendelea kupambana na changamoto hiyo.
“Tumekuwa na mapumziko ya wiki tatu kabla ya kurejea katika mechi za ushindani, mwenendo wetu kiujumla sio mzuri, lakini tunaendela kujifunza kutokana na makosa, kwa sababu wachezaji wengi ni vijana na wanahitaji pia muda,” amesema Chipo wakati akizungumza.K
Kocha huyo aliyejiunga na timu hiyo Novemba 17, 2025, amepoteza mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu, baada ya kuchapwa mabao 3-1 dhidi ya Mashujaa na Singida Black Stars, kisha 3-0 mbele ya Azam FC, huku ikifunga bao moja na kuruhusu tisa.
Katika mechi 16, ilizozicheza msimu huu, Mtibwa Sugar imeshinda tano, sare sita na kupoteza tano, ikiwa nafasi ya nane na pointi 21, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho ikifunga mabao 13 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 17.
Nyota anayeongoza kwa kufunga mabao mengi ya Ligi Kuu katika timu hiyo ni Fredrick Magata, aliyefunga matatu hadi sasa, akifuatiwa na Ismail Mhesa na Said Mkopi wenye mawili kila mmoja, huku mshambuliaji Raizin Hafidh, akifunga bao moja.
Chipo aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo za Pamba Jiji, Coastal Union na TRA United zamani Tabora United, alijiunga na kikosi hicho, Novemba 17, 2025, baada ya kuachana na Murang’a SEAL ya kwao Kenya tangu, Agosti 21, 2025.
Kocha huyo anakumbukwa na mashabiki hasa baada ya kukiongoza kikosi cha Ulinzi Stars kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu ya Kenya ‘KPL’ kati ya 2003 na 2005 na kuhudumu akiwa kocha msaidizi wa Harambee Stars kuanzia 2008 hadi 2011.