Amorim, Man United mulemule
![](/resource/image/4914824/landscape_ratio2x1/320/160/fd92e7724989192f565024ad7f71c47a/Lz/man-u-pc.jpg)
Muktasari:
- Ni ngumu kuamini kwamba Amorim alichohitaji ni kumsajili beki wa kushoto tu na yule beki kinda wa kutoka Arsenal - hata kama alifurahia kwa kitendo cha kuwaondoa Marcus Rashford na Antony kwenye kikosi chake.
MANCHESTER, ENGLAND; PRESHA ipo juu kwa kocha Ruben Amorim baada ya dirisha la usajili la majira ya baridi huko Ulaya kufungwa huku chama lake la Manchester United likishindwa kunasa mastaa wa maana wa kuja kuongeza nguvu kikosini.
Ni ngumu kuamini kwamba Amorim alichohitaji ni kumsajili beki wa kushoto tu na yule beki kinda wa kutoka Arsenal - hata kama alifurahia kwa kitendo cha kuwaondoa Marcus Rashford na Antony kwenye kikosi chake.
Pesa inaonekana kuwa kikwazo kikubwa kwa Man United kushindwa kuwa na nguvu kubwa kwenye soko la usajili, licha ya kikosi chao kuwa na shida nyingi ndani ya uwanja hadi sasa msimu ulipofika. Mashabiki wengi wa Man United walimtaka kocha Amorim na mabosi wake kufanya usajili kwenye dirisha dogo.
Hata hivyo, pamoja na ishu ya kifedha, pengine Amorim na Man United imeamua kupita njia ambazo Liverpool na Arsenal imepita hadi kufikia ubora wa sasa.
Mabadiliko yanahitaji muda. Ni suala la kuhitaji usahihi na sio kufanya tu ilimradi, kila kitu kizuri kinahitaji muda.
Man United, ambayo kwa sasa ipo nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu England pengine itahitaji kufanya kwa ubora zaidi kuliko wapinzani wao wa Anfield na Emirates wakati zilipokuwa katika kipindi cha mabadiliko. Makocha Jurgen Klopp na Mikel Arteta, walifanya kazi kubwa kufanya mabadiliko kwenye timu za Liverpool na Arsenal walipoingia kwa mara ya kwanza na hicho ndicho kitu Amorim anataka kukifanya Man United.
Klopp alitua Anfield akirithi kikosi cha Brendan Rodgers kilichokuwa na shida nyingi. Mechi yake ya kwanza alitoka sare ya bila kufungana dhidi ya Tottenham Hotspur, huku timu yake ilikuwa na wachezaji kama Martin Skrtel, Mamadou Sakho na Alberto Moreno kwenye beki, Emre Can na Lucas Leiva kwenye kiungo na benchini alikuwa na wachezaji Jordan Ibe, Jerome Sinclair na Kolo Toure.
Kitu cha kwanza kufanya Klopp, alianza kubadili akili za wachezaji kwanza aliowakuta kwenye kikosi kabla ya kuanza kuwafungulia mlango wa kutokea mmoja baada ya mwingine. Na Liverpool usajili pekee iliyofanya Januari 2006, ilikuwa kumnasa kiungo Marko Grujic na ikamtoa kwa mkopo Red Star Belgrade.
Ilipofika dirisha kubwa, wachezaji 16 - wakiwamo wasiopungua sita ambao walicheza mechi ile ya Spurs, walifunguliwa mlango wa kutokea na hapo wakaletwa Joel Matip, Sadio Mane na Georginio Wijnaldum, wakiwa miongoni mwa nguvu mpya zilizoongezwa kwenye timu. Jambo hilo lilikwenda sambamba na kuwajenga wachezaji utimamu wao wa mambo ya nje ya uwanja, mazoezini na kwenye vyumba vya kubadilishia.
Baada ya hapo Klopp alijifunza kutambua majina ya wafanyakazi wote 80 wa Liverpool waliopo kwenye uwanja wao wa mazoezi huko Melwood na kisha kuwatambulisha kwa wachezaji. Hiyo ilileta msikamano na kuibuka na kauli mbinu yao ‘One club. One goal’. Kwamba umoja wao unaanzia kwa mfanyakazi wa kawaida wa kutunza nyasi za uwanjani hadi kwa straika wa timu hiyo ambaye ni staa. Ukapatikana mshikamano.
Kama ilivyo kwa Arsenal, Arteta, aliteuliwa kabla ya Krismasi 2019, aliishia kunasa mchezaji wa mkopo kwenye dirisha lake la kwanza la usajili.
Akanasa mastaa watatu, huku Emile Smith Rowe na beki Mavropanos wakaondoka kwa muda.
Mabadiliko makubwa ya klabu yalikuja baada ya hapo. Januari waliwasili Pablo Mari na Cedric Soares ambao dili zao za mkopo zikafanywa za jumla, huku beki wa Kibrazili Gabriel, kiungo Thomas Partey na winga Willian waliongezwa kikosini.
Na safisha safisha ilianza kueleweka kwenye dirisha lake la pili na tatu, ambapo Henrikh Mkhitariyan, Mesut Ozil na mabeki Sokratis na Mustafi wote waliondoka Januari 2021 na wakafuatiwa na straika Pierre-Emerick Aubameyang.
Ilipofika Agosti 2022, chini ya miaka mitatu tangu alipotua Emirates, wachezaji watano tu ndiyo waliokuwa na uhakika wa nafasi kwenye timu yake, ambao ni Bukayo Saka, Smith Rowe, Granit Xhaka, Gabriel Martinelli na Reiss Nelson - ambapo timu hiyo ilijijenga na kuwa ya kiushindani kwa sasa.
Kama ilivyokuwa kwa Klopp, hata Arteta naye alijali kwenye kuvumilia na kuijenga timu kuwa ya viwango kuliko kuhitaji mabadiliko ya haraka.
Wakati anatimiza miaka yake mitano kwenye kikosi cha Arsenal, Desemba mwaka jana, Arteta alisema: “Kitu cha kwanza nilifanya ni kutengeneza umoja kwenye timu kuanzia kwa wafanyakazi hadi kwa wachezaji, niliwaambia ninachofikiria na kama tutashindwa kukifanya, basi tutashindwa kufikia mafanikio.”
Kwa Arteta na Klopp hawakuwa na nyakati ngumu sana kulinganisha na Amorim. Klopp alipoteza mechi moja tu kati ya 11 za kwanza, wakati Arteta alipoteza moja katika mechi 14. Kwa Amorim mambo ni tofauti, amepoteza mechi sita kati ya 11 za kwanza tangu alipochukua mikoba ya Erik ten Hag.
Mambo yamekuwa magumu, kwa ujumla wake timu hiyo imeshinda mara nane katika mechi 19, imepata ushindi mara nne tu katika mechi 13 za mwisho, huku ikipoteza mara saba katika Ligi Kuu England. Kubadilibadili kikosi inatajwa kuwa sababu nyingine, ambapo mfano kwenye mechi dhidi ya Crystal Palace, Jumapili iliyopita aliamua kucheza na Namba 9 bandia, alipomtumia kiungo Kobbie Mainoo na kuwaacha benchini mastraika wa asili, Joshua Zirkzee na Rasmus Hojlund. Usajili wake mkubwa aliofanya Amorim kwenye dirisha lililopita ni beki wa kushoto, Patrick Dorgu.
Rekodi zinaonyesha kwamba Klopp msimu wake wa kwanza Liverpool, timu ilimaliza nafasi ya nane, sawa na Arteta, naye timu yake ilimaliza namba nane.
Mechi ya kwanza ya Klopp (Liverpool vs Spurs): Mignolet; Clyne, Skrtel, Sakho, Moreno; Coutinho (Ibe), Can, Milner, Lallana (Allen), Lucas; Origi
Mechi ya kwanza ya Arteta (Arsenal vs Everton): Leno; Chambers, Luiz, Maitland-Niles, Saka; Torreira, Smith Rowe (Willock), Xhaka; Martinelli, Aubameyang (Lacazette), Nelson