Arsenal ikikaza tu inachukua EPL!
Muktasari:
- Kuna kitu kinapikwa kwenye mchakamchaka wa kusaka taji la Ligi Kuu England, ishakusanya pointi 22 katika mechi tisa. Lakini, kwa misimu sita iliyopita, Arsenal imekuwa ikivuna pointi 22 au zaidi katika mechi tisa za kwanza, hivyo ni kawaida yao.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL inachokifanya, ilishakifanya, lakini safari hii mambo yanaonekana kama yapo tofauti.
Kuna kitu kinapikwa kwenye mchakamchaka wa kusaka taji la Ligi Kuu England, ishakusanya pointi 22 katika mechi tisa. Lakini, kwa misimu sita iliyopita, Arsenal imekuwa ikivuna pointi 22 au zaidi katika mechi tisa za kwanza, hivyo ni kawaida yao.
Hata hivyo, mara hizo zote sita ilipokuwa kwenye ubora huo, imeshinda taji la Ligi Kuu England mara moja tu, msimu ule ambao ilicheza bila ya kupoteza 2003-04.
Kwa sasa mambo yapo vizuri chini ya Mikel Arteta. Timu yake ni bora na kikosi kipo imara, huku wapinzani wake wa nguvu kwenye vita ya ubingwa, hali zao si nzuri na waamuzi hawafanyi sana makosa msimu huu, hivyo kunaweza kutokea jambo Emirates.
Kocha asiyeishiwa maneno, Jose Mourinho mwaka 2014 alimwambia gwiji wa Arsenal, Arsene Wenger “speshalisti wa kufeli” ingawa maneno hayo yalionekana makali, lakini yalibeba ukweli ndani yake, amesema baada ya Arsenal kuwa na ukame wa mataji tangu ilipobeba Kombe la FA mwaka 2005. Na ukiitazama Arsenal hii iliyomaliza nafasi ya pili kwa misimu mitatu mfululizo, Mourinho angeweza kusema kauli kama ile ya Wenger kwa Arteta.
Kitu kizuri kuhusu Arsenal hii ya Arteta, hasa ya msimu huu ni ngumu kufungika. Na ndiyo maana kuna matumaini makubwa ya kunyakua taji la Ligi Kuu England.
Arteta alipewa zaidi ya Pauni 1 bilioni kusajili wachezaji, huku robo ya pesa hiyo ilitumika kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka huu, aliposawasajili washambuliaji Viktor Gyokeres, Eberechi Eze na Noni Madueke. Martin Zubimendi naye ametua kuja kuimarisha kwenye kiungo ya kukaba na mambo ni mazuri kuna mechi za kutosha za kutoruhusu bao.
Arsenal imecheza mechi tano mfululizo bila ya kuruhusu bao na mechi nne za mwisho imeruhusu wapinzani wao kupiga mashuti mawili tu yaliyolenga goli lao.
Ujio wa beki wa zamani wa Manchester United, Gabriel Heinze kwenye benchi la ufundi la kikosi cha kwanza limekuwa ongezeko muhimu. Heinze ana kazi moja ya kufundisha timu hiyo namna bora ya kukaba na hivyo kuifanya ngome ya Arsenal kuwa isiyopenyeka kirahisi. Ukuta mgumu.
Silaha nyingine ya Arsenal ni uhodari wa kutumia mipira iliyokufa. Eneo hilo pia kuna mtu wake maalumu, Nicolas Jover, ambaye ameifanya Arsenal kuwa tishio kwenye mipira ya aina hiyo, ikifunga mabao mengi kwa mipira ya aina hiyo kuliko timu nyingine kwenye Ligi Kuu England.