Arteta namba zinatosha

Muktasari:
- Kwa kuzingatia hilo, rekodi ya mechi 200 za kwanza za kocha Arteta kwenye Ligi Kuu England zimelinganishwa na makocha wengine mashuhuri kwenye ligi hiyo, Pep Guardiola, Jurgen Klopp, Arsene Wenger, Sir Alex Ferguson, Jose Mourinho na Rafa Benitez walivyofanya kwenye mechi zao 200 za kwanza kwenye mikikimikiki hiyo.
LONDON, ENGLAND: MIKEL Arteta ametimiza mechi 200 za Ligi Kuu England tangu alipochukua mikoba ya kuinoa Arsenal mwaka 2019 – lakini rekodi zake zinachuana vipi na makocha wanaotajwa kuwa manguli kwenye historia ya michuano hiyo?
Kwa kuzingatia hilo, rekodi ya mechi 200 za kwanza za kocha Arteta kwenye Ligi Kuu England zimelinganishwa na makocha wengine mashuhuri kwenye ligi hiyo, Pep Guardiola, Jurgen Klopp, Arsene Wenger, Sir Alex Ferguson, Jose Mourinho na Rafa Benitez walivyofanya kwenye mechi zao 200 za kwanza kwenye mikikimikiki hiyo.
Arteta alichukua mikoba ya kuinoa Arsenal, Desemba 2019 na mwanzoni alipata shida kuipa timu hiyo matokeo mazuri hadi hapo mambo yalipokuja kukaa vizuri.

Na hakika, kocha huyo Mhispaniola aligeuza Arsenal kuwa timu bora kabisa na kushindania mataji ya Ligi Kuu England kwenye msimu wa 2022-23 na 2023-24.
Na msimu huu, Arsenal ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, pointi 15 nyuma ya vinara Liverpool, hiyo ina maana Arteta ameweza kushikilia kile ambacho amekifanya kwa misimu mitatu iliyopita katika msako wa kuwania taji katika kikosi hicho chenye maskani yake Emirates.
Kwa kushinda mechi 118 kati ya 199 za kwanza — ushindi wa mechi tano zaidi ya makocha wengine waliopita kwenye mechi zao 200 za kwanza kwenye Ligi Kuu England — Arteta amejipambanua kama mmoja wa makocha wenye mafanikio makubwa katika kizazi chake.

Anaburuzwa na Guardiola, Mourinho, Klopp na Ferguson kwenye upanda wa wastani wa ushindi katika mechi hizo 200 za kwanza kwenye ligi.
“Najivunia kufikia hatua hii, lakini ninachowaza ni hatima yangu sasa,” alisema Arteta kabla ya kuwakabili Manchester United uwanjani Old Trafford, juzi.