Arteta: Real Madrid wepesi tu

Muktasari:
- Arteta anaamini itakuwa ngumu kushinda mbele ya Madrid ambao ni mabingwa mara 15 wa Ligi ya Mabingwa lakini bado inawezekana.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal Mikel Arteta amewatia moyo na kuwataka wachezaji wake kujiandaa vilivyo kuelekea mchezo wao ujao wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Real Madri baada ya kufanikiwa kuitoa PSV wiki hii.
Arteta anaamini itakuwa ngumu kushinda mbele ya Madrid ambao ni mabingwa mara 15 wa Ligi ya Mabingwa lakini bado inawezekana.
"Ni vigumu sana lakini tuna uwezo wa kufanya hivyo," alisema Arteta baada ya kuifunga PSV Eindhoven na kufika robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo.
Washika mitutu hawa kutoka London, msimu uliopita, walitolewa na Bayern Munich katika hatua ya robo na mwezi ujao watakuwa tena kwenye changamoto kubwa dhidi ya Real Madrid ambao walipata ushindi kwa mikwaju ya penati dhidi ya Atletico Madrid.
"Tuko robo fainali za Ligi ya Mabingwa kwa msimu wa pili mfululizo na tunapaswa kutambua kwamba ni vigumu kufanya hivyo," alisema Arteta. "Sasa tunataka kuchukua hatua inayofuata zaidi ya hapa."
"Ni muhimu, kwa sababu tunataka kushinda mataji, kwa sababu timu pia inahitaji hilo, sisi ni klabu inayotaka kuwa bora na inataka kushindana na timu nyingine bora duniani."
"Ili kufanya hivyo lazima uwepo kila wakati na ni vigumu sana, lakini tumefanya hivyo kwa miaka miwili mfululizo na tuna uwezo na uwezo wa kufanya bora zaidi."
Arsenal imepita kwa jumla ya mabao 9-3 baada ya mchezo wa kwanza kushinda 7-1 kisha mchezo wa wiki ikatoka sare ya mabao 2-2.