Baada ya Mexico, sasa ni zamu ya Canada na Marekani
Muktasari:
- Kabla ya mechi hiyo ambayo itapigwa saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kwenye dimba la BMO, leo alfajiri imeshuhudiwa mechi ya kufunga hesabu ya raundi ya kwanza kwa kundi A saa 11:00 alfajiri kati ya Korea Kusini dhidi ya Jamhuri ya Czech.
TORONTO, CANADA: BAADA ya kushuhudia wenyeji wenza wa fainali za Kombe la Dunia, Mexico wakitoana jasho dhidi ya Afrika Kusini katika mchezo wa ufunguzi, macho ya mashabiki sasa yanaelekezwa nchini Canada ambako wenyeji hao wanashuka dimbani leo, Ijumaa, kuwakaribisha Bosnia na Herzegovina katika mechi ya kwanza ya Kundi B.
Kabla ya mechi hiyo ambayo itapigwa saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kwenye dimba la BMO, leo alfajiri imeshuhudiwa mechi ya kufunga hesabu ya raundi ya kwanza kwa kundi A saa 11:00 alfajiri kati ya Korea Kusini dhidi ya Jamhuri ya Czech.
Yani wakati huku kukikucha huko Mexico hesabu za raundi ya kwanza ya kundi A zimefungwa kila timu imesaliwa na mechi mbili tu za kupigania nafasi ya kwenda hatua ya mtoano.
Canada ambao watacheza kwenye ardhi yao ya nyumbani, wanaingia kwenye mashindano haya wakiwa na matumaini makubwa ya kuandika historia mpya mbele ya mashabiki wao baada ya kushindwa kufanya vizuri katika ushiriki wao wa awali wa Kombe la Dunia.
Taifa hilo limewahi kushiriki fainali hizo mara mbili, mwaka 1986 na 2022 lakini likapoteza mechi zote sita lilizocheza katika mashindano hayo. Hata hivyo, kikosi cha kocha Jesse Marsch kina sababu za kujiamini kutokana na rekodi nzuri nyumbani. Canada wamekuwa wagumu kufungika mjini Toronto ambapo wamepoteza mchezo mmoja tu katika mechi zao 28 za mwisho za kimataifa, jambo linalowapa matumaini ya kuanza vizuri michuano hiyo.
Kwa upande wa Bosnia na Herzegovina, huu ni ushiriki wao wa pili katika Kombe la Dunia baada ya kuonekana kwa mara ya kwanza nchini Brazil mwaka 2014. Ingawa walitolewa hatua ya makundi wakati huo, safari yao ya kufuzu kwa fainali hizi imeonyesha ukuaji mkubwa wa timu hiyo ambayo ilipoteza mechi moja tu katika michezo minane ya awali ya kufuzu kabla ya kupita hatua za mtoano.
Bosnia wanaingia kwenye pambano hili wakiwa katika kiwango kizuri baada ya kucheza mechi nane mfululizo bila kupoteza. Wameonyesha uwezo mkubwa wa kushambulia kwa kufunga katika kila moja ya mechi zao 10 za kufuzu huku kocha Sergej Barbarez akiamini kikosi chake kinaweza kuanza vizuri dhidi ya wenyeji hao.
Mchezo huu pia utaingia kwenye vitabu vya historia kwani utakuwa wa kwanza kabisa kwa Canada na Bosnia kukutana katika mashindano yoyote ya kimataifa, jambo linaloongeza hamasa na kutokuwa na uhakika wa matokeo.
Macho mengi yatakuwa kwa mshambuliaji nyota wa Canada, Jonathan David, ambaye ndiye mfungaji bora wa muda wote wa taifa hilo akicheka na nyavu mara 39 katika mechi 75 za kimataifa na amehusika moja kwa moja katika mabao matano kwenye mashindano makubwa mawili yaliyopita.
Bosnia wao wanamtegemea mkongwe Edin Dzeko ambaye licha ya kutimiza miaka 40 bado anaendelea kuwa tishio, akiwa mfungaji bora wa muda wote wa taifa hilo kwa mabao 68 katika mechi 141 za kimataifa.
Hata hivyo, Canada wanaweza kuikosa huduma ya nahodha wao Alphonso Davies ambaye bado hajawa fiti kwa asilimia 100, wakati Bosnia wamepata nafuu baada ya mshambuliaji Haris Tabakovic kusafiri na kikosi licha ya kusumbuliwa na majeraha.
TUTAKESHA MAREKANI
Baada ya mchezo kati ya Canada na Bosnia kupigwa, itakuwa ni muda mfupi wa kupumzika kabla ya mashabiki kushuhudia mchezo mwingine wa kusisimua alfajiri ya Jumamosi saa 10:00, ambapo Marekani watawakaribisha Paraguay katika mchezo wa Kundi D hilo.
Marekani wamesonga hatua ya 16 bora walipokuwa wenyeji wa Kombe la Dunia mwaka 1994 na wana kila sababu ya kujiamini kurudia mafanikio hayo, baada ya kufika hatua ya mtoano katika kila moja ya mashindano yao matatu ya mwisho (2010, 2014 na 2022).
Katika mechi zao tisa za mwisho za hatua ya makundi, Marekani wamepoteza mchezo mmoja pekee dhidi ya mabingwa wa 2014, Ujerumani (W3, D5, L1). Hata hivyo, kuendeleza rekodi yao ya kutopoteza mechi ya kwanza ya hatua ya makundi tangu mwaka 2010 (W1, D2) kunaweza kuwa mtihani mgumu safari hii, kwani kikosi cha Mauricio Pochettino kinaingia kwenye mashindano kikiwa kimeshinda mchezo mmoja pekee kati ya michezo minne walizocheza mwaka 2026 (W1, L3), ingawa yote ilikuwa dhidi ya timu zilizopo juu yao katika viwango vya FIFA.
Kwa upande wa Paraguay, wao wamekuwa katika kiwango kizuri baada ya kushinda mechi tatu kati ya nne za mwisho (L1) na wanarejea Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2010 baada ya kuwa na wakati mzuri katika michezo ya kufuzu ya CONMEBOL.