Balaa la Europa... Man United yapewa wabishi, Spurs kicheko

Muktasari:
- Klabu hizo mbili zitakazowakilisha Ligi Kuu England kwenye michuano hiyo zilitinga hatua ya mtoano baada ya kumaliza kwenye nafasi nane za juu katika hatua ya makundi.
NYON, USWISI: KUMEKUCHA. Manchester United na Tottenham Hotspur zimeshafahamu njia zitakazopita katika kufukuzia ubingwa wa Europa League baada ya droo ya hatua ya mtoano ya 16 iliyopangwa Ijumaa huku kukiwa na uwezekano wa kukutana na madui zao kwenye robo fainali na nusu fainali.
Klabu hizo mbili zitakazowakilisha Ligi Kuu England kwenye michuano hiyo zilitinga hatua ya mtoano baada ya kumaliza kwenye nafasi nane za juu katika hatua ya makundi.
Na sasa kwenye mtoano huo, Man United ya Ruben Amorim itacheza na Real Sociedad, timu ambayo inafahamiana nayo vyema baada ya kukutana kwenye hatua ya 32 bora ya Europa League msimu wa 2020-21 na zilikutana pia kwenye hatua ya makundi msimu wa 2022-23, ambapo ilipoteza Old Trafford 1-0 na kwenda kushinda kwa idadi kama hiyo ya bao ugenini.
Kama Man United itafuta hatua hiyo itakwenda kuchuana na ama Lyon au FCSB kwenye hatua ya robo fainali, jambo ambalo kwenye karatasi linaonekana kuwa jepesi kufika nusu fainali.
Rangers itakipiga na Fenerbahce ya Jose Mourinho kwenye mechi nyingine ya hatua ya 16 bora, kwenye droo hiyo ambapo kocha huyo Mreno, akipenya anaweza kukutana na waajiri wake wa zamani kwenye nusu fainali.
Mechi nyingine, Ajax itakipiga na Eintracht Frankfurt, FCSB na Lyon, Viktoria Plzen na Lazio na AS Roma itamalizana na Athletic Bilbao. Spurs imepewa kisiki za Uholanzi, wakati itakapoikabili AZ Alkmaar, timu ambayo ilikutana nayo kwenye hatua ya makundi na kushinda 1-0.
Na kama kikosi hicho cha kocha Ange Postecoglou kikipenya hatua hiyo, kitaenda kumenyana na ama Eintracht Frankfurt au Ajax kwenye hatua inayoafuata, kitu ambacho kinaweza kurudisha kumbukumbu ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika msimu wa 2018-19.
Mechi za kwanza za hatua ya 16 bora za kwanza zitapigwa Machi 6 na 13, wakati robo fainali ni Aprili 10 na 17. Nusu fainali itapigwa Mei 1 na 8, wakati fainali yenyewe itachezwa San Mames, Mei 21.
RATIBA YENYEWE YA EUROPA
Bodo/Glimt vs Olympiacos
Fenerbahce vs Rangers
Ajax vs Eintracht Frankfurt
FCSB vs Lyon
AZ Alkmaar vs Tottenham
Real Sociedad vs Man United
Viktoria Plzen vs Lazio
Roma vs Athletic Bilbao
ROBO FAINALI:
Viktoria Plzen/Lazio vs Bodo/Glimt vs Olympiacos
Ajax/Frankfurt vs AZ Alkmaar vs Tottenham
Roma/Bilbao vs Fenerbahce/Rangers
FCSB/Lyon vs Sociedad/Man United