Prime
Balaa la majeruhi... Arteta apewa mastraika sita

Muktasari:
- Gabriel Jesus hataonekana uwanjani hadi mwisho wa msimu, wakati Bukayo Saka bado hayupo fiti kurudi uwanjani baada ya kufanyiwa upasuaji wa misuli. Wakati Gabriel Martinelli akitarajia kukosekana kwa miezi kadhaa, Kai Havertz naye ameumia na atakuwa nje hadi mwisho wa msimu.
LONDON, ENGLAND: MAJERUHI yameipiga pabaya Arsenal na sasa inahaha namna ya kuboresha fowadi yao.
Gabriel Jesus hataonekana uwanjani hadi mwisho wa msimu, wakati Bukayo Saka bado hayupo fiti kurudi uwanjani baada ya kufanyiwa upasuaji wa misuli. Wakati Gabriel Martinelli akitarajia kukosekana kwa miezi kadhaa, Kai Havertz naye ameumia na atakuwa nje hadi mwisho wa msimu.
Jambo hilo linaifanya Arsenal kuwa na pengo kubwa la kuziba kwenye safu yao ya ushambuliaji.
Arsenal ilikuwa na nafasi ya kusajili kwenye dirisha la Januari, lakini ilishindwa kunasa saini yoyote. Ilikwama kweye mpango wao wa kumsajili straika Ollie Watkins, hivyo ikaamua kufuta kabisa mpango wa usajili kwenye dirisha hilo dogo, wakisubiri mwisho wa msimu.
Lakini, baada ya kukumbwa na janga hilo la majeruhi wengi wa safu ya ushambuliaji kwenye kikosi chao, kocha Mikel Arteta bado kuna kitu anaweza kukifanya kwenye usajili ili apate fowadi mpya.
Arsenal ni moja ya timu kwenye Ligi Kuu England, ambayo haijakamilisha idadi ya wachezaji 25 wanaotakiwa kwenye kikosi, hivyo inaweza kufanya usajili wa wachezaji huru kuokoa jahazi.
Kutokana na hilo, hii hapa orodha ya mastraika huru waliopo sokoni kwa sasa ambao Arsenal inaweza kuwasajili bure kabisa kipindi hiki ambacho dirisha la usajili limefungwa.

- Mariano Diaz
Akiwa na umri wa miaka 31 kwa sasa, Mariano alicheza Real Madrid kwa awamu mbili tofauti na zote zilikuwa za miamba hiyo kutamba kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya 2017 na 2022. Amekuwa hana timu tangu alipoondoka Sevilla mwishoni mwa msimu uliopita, huku akiwahi kukabiliana na Arsenal kwenye mechi mbili za michuano ya Ulaya msimu uliopita.

2. Maxi Gomez
Straika wa Uruguay, Gomez alikuwa sehemu ya kikosi cha nchi hiyo kilichocheza kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022. Amefunga mabao 50 kwenye La Liga wakati alipokuwa akikipiga Celta Vigo na Valencia. Gomez, 28, aliachana na Trabzonspor kwenye dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana na msimu uliopita alikuwa kwa mkopo Cadiz. Bado ana ujuzi mkubwa uwanjani.

3. Carlos Vela
Jina maarufu kabisa kwenye uzi wa Arsenal na staa huyo aliibukia kutoka kwenye timu hiyo na kumbukumbu kubwa ni kuhusu hat-trick yake 2008. Baada ya kuondoka Arsenal, Vela alienda Hispania kabla ya kutimkia Ligi Kuu Marekani kwenye kikosi cha Los Angeles FC, ambako amekuwa kinara wa mabao wa muda wote akifunga mara 78 katika mechi 152 za ligi.

4. Lucas Perez
Staa mwingine wa zamani wa Arsenal, Perez alifunga hat-trick katika mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika msimu wake wa kwanza na timu hiyo, lakini aliondoka 2018 baada ya kucheza mechi 21. Akiwa na umri wa miaka 36, Perez aliachana na Deportivo La Coruna kwa matatizo binafsi Januari, Arsenal inaweza kujaribu kunasa saini yake.

5. Diego Costa
Wolves ilijikuta kwenye balaa kama lililoikumba Arsenal kwa sasa mwaka 2022 wakati straika Sasa Kalajdzic aliumia goti na kumazimika kwenda kumsajili Diego Costa. Na sasa Arsenal inaweza kurudi kwa straika huyo wa zamani wa Chelsea kuja kuokoa jahazi kwa muda hadi mwisho wa msimu. Kufunga mabao haijawahi kuwa tatizo kwa mshambuliaji huyo.

6. Leandro Damiao
Mbrazili huyo alikuwa kwenye rada za klabu za Ligi Kuu England kipindi hicho alipokuwa kinda na Tottenham ilitajwa sana kuhitaji saini yake. Lakini, sasa akiwa ametimiza umri wa miaka 35, hana timu tangu alipoachana na Coritiba na kuelezwa alihitaji kurudi kwenye klabu yake ya zamani ya Internacional. Arsenal sasa inaweza kunasa saini ya mchezaji huyo kwa muda.