Balikwisha, Kalimuendo kuongeza nguvu DR Congo
Muktasari:
- Miongoni mwa majina yanayotajwa kwa sasa ni mshambuliaji wa Celtic, Michel-Ange Balikwisha ambaye anaonekana kuwa mmoja wa silaha mpya zinazotazamwa kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji.
KINSHASA, DR CONGO: WAKATI DR Congo ikiwa na hesabu za maandalizi ya kutosha kuelekea Kombe la Dunia 2026, shirikisho la soka la nchi hiyo, FECOFA linaendelea na mkakati wa kuwavuta wachezaji wenye asili ya Congo wanaocheza soka la kulipwa Ulaya ili kuongeza ushindani katika kikosi cha Kocha Sebastien Desabre.
Miongoni mwa majina yanayotajwa kwa sasa ni mshambuliaji wa Celtic, Michel-Ange Balikwisha ambaye anaonekana kuwa mmoja wa silaha mpya zinazotazamwa kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji.
Balikwisha, 24, alizaliwa Ubelgiji lakini ana asili ya DR Congo. Kabla ya kuhamia Celtic mwaka 2025 alikuwa akiichezea Antwerp ya Belgium na msimu uliopita katika mechi za mchujo wa ubingwa, alifunga mabao manne na kutoa asisti tatu katika mechi 10.
Katika maisha yake ya klabu mpaka sasa, Balikwisha amecheza mechi 198 za kulipwa, akifunga mabao 39 na kutoa pasi 23 za mabao akiwa amepitia Standard Liege, Antwerp na sasa Celtic.
Taarifa kutoka Scotland zinaeleza kuwa tayari Balikwisha amefanya uamuzi wa kuichezea DR Congo na hatua hiyo imeonekana kuwa ushindi mkubwa kwa Desabre ambaye amekuwa akiwafuatilia wachezaji wa diaspora wanaocheza Ulaya.
Mbali na Balikwisha, jina lingine linalotajwa kwa nguvu ni Arnaud Kalimuendo ambaye kwa sasa anakipiga England baada ya kuhamia Nottingham Forest akitokea Rennes ya France.
Kalimuendo ambaye aliwahi kuchezea timu za vijana za Ufaransa, bado hajacheza mechi rasmi timu kubwa ya taifa hilo jambo linaloifanya DR Congo kuendelea kuwa na matumaini ya kumpata.
Mshambuliaji, 23, alikuwa moto msimu uliopita akiwa Rennes na alifunga mabao 18 na kutoa asisti nne katika mechi 34 za mashindano yote kabla ya kusajiliwa Nottingham Forest kwa dau linaloripotiwa kufikia Pauni 26 milioni.
Kwa jumla yake akiwa Rennes, Kalimuendo alifunga mabao 40 katika mechi 112, rekodi iliyomfanya kuingia kwenye rada za klabu kadhaa za England kabla ya Forest kushinda vita hiyo ya usajili.