Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

England yafuzu 32 bora Kombe la Dunia ikiacha maswali

Muktasari:

  • Ushindi wa mabao 2-0 ambao wameupata  umeihakikishia England kukutana na DR Congo katika hatua inayofuata, lakini kama itacheza kwa kiwango  ilichoonyesha  kwenye hatua ya makundi, safari yake inaweza kuisha mapema kuliko ilivyotarajiwa.

VIJANA wa Thomas Tuchel, England wamekamilisha kazi ya kwanza baada ya kumaliza vinara wa Kundi L na kufuzu hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026, lakini kiwango walichoonyesha dhidi ya Panama kimracha maswali kuhusu uwezo wa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Ushindi wa mabao 2-0 ambao wameupata  umeihakikishia England kukutana na DR Congo katika hatua inayofuata, lakini kama itacheza kwa kiwango  ilichoonyesha  kwenye hatua ya makundi, safari yake inaweza kuisha mapema kuliko ilivyotarajiwa.

Tuchel ameendelea kusisitiza kuwa timu yake itakuwa bora kadri mashindano yanavyozidi kuwa magumu.

Hata hivyo, mechi dhidi ya Panama imeonyesha bado kuna upungufu mkubwa unaohitaji kurekebishwa kabla ya kukutana na wapinzani wenye uwezo mkubwa zaidi.

Kwa zaidi ya saa moja ya mchezo, England ilishindwa kuivunja safu ya ulinzi ya Panama, timu ambayo iko nafasi ya 42 kwenye viwango vya FIFA.

Hata ilipopata ushindi, haikuwa kwa sababu ilitawala mchezo kwa urahisi, bali kutokana na ubora wa wachezaji  binafsi waliobadili matokeo.

BELLINGHAM AIBEBA ENGLAND

Kwa mara nyingine, Jude Bellingham ameonyesha kwa nini ni mmoja wa wachezaji muhimu zaidi ndani ya kikosi cha England.

Kabla ya mashindano kulikuwa na mjadala kama anastahili kuanza mbele ya Morgan Rogers, lakini Tuchel aliamua kuendelea kumwamini kutokana na uzoefu wake katika mechi kubwa.

Dhidi ya Panama, uamuzi huo umeonekana kuwa sahihi kwani ndiye aliyefungua mchezo kwa kufunga bao la kwanza kabla ya kutoa krosi iliyomsaidia Harry Kane kufunga la pili.

Uwezo wake wa kutengeneza nafasi, kupambana katikati ya uwanja na kuibeba timu katika nyakati ngumu ulimfanya kuwa Mchezaji Bora wa Mechi.

Katika mechi ambazo England imepata ushindi dhidi ya Croatia na Panama, mchango wa Bellingham umekuwa wa moja kwa moja.

Kama England ina ndoto ya kutwaa Kombe la Dunia, itahitaji kiwango kama hicho kutoka kwa kiungo huyo hadi mwisho wa mashindano.


KANE AENDELEA KUVUNJA REKODI

Kane ameendelea kuthibitisha ubora  kwa kufunga bao lililomfanya kuwa mfungaji bora zaidi wa England katika historia ya fainali za Kombe la Dunia akiwa na mabao 11, akimpita Gary Lineker aliyekuwa na 10.

Mbali na mabao, Kane ameendelea kuwa kiongozi wa safu ya ushambuliaji na mshirika muhimu wa Bellingham, jambo ambalo linaipa England matumaini ya kuwa na safu ya ushambuliaji yenye uwezo wa kuamua mechi kubwa.

RASHFORD ATUMA UJUMBE KWA TUCHEL

Marcus Rashford alipewa nafasi ya kuanza badala ya Anthony Gordon na aliitumia vizuri akiwa mchezaji mwenye kasi zaidi kipindi cha kwanza, akimlazimisha kipa wa Panama kufanya makosa huku akikaribia kufunga kupitia kichwa na mpira wa adhabu.

Ingawa hakufunga, alionyesha anaweza kuwa chaguo bora zaidi katika mechi zijazo, jambo ambalo linaweza kumlazimisha Tuchel kuendelea kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.


UKUTA HAUPO SAWA

Pamoja na ushindi huo, eneo linalotia wasiwasi zaidi England ni safu ya ulinzi.

England iliiruhusu Panama kutengeneza nafasi nyingi za kufunga huku mabeki wakionekana kukosa maelewano. Panama ilipata mashambulizi kadhaa ya hatari na hata kufunga bao lililokataliwa kutokana na kuotea.

Hali hiyo inaonyesha kuwa dhidi ya timu zenye washambuliaji wa kiwango cha juu, England inaweza kuadhibiwa kirahisi ikiwa haitaimarisha ulinzi wake.


MASWALI KUHUSU MABEKI PEMBENI

Uamuzi wa Tuchel katika nafasi za mabeki wa pembeni pia umeendelea kuzua mjadala.

Majeraha ya Reece James pamoja na kumtumia Jarell Quansah, ambaye kiasili ni beki wa kati, katika nafasi ya beki wa kulia, yanaonyesha kuwa England bado haijapata suluhisho eneo hilo.

Iwapo matatizo hayo yataendelea dhidi ya timu zenye kasi na ubora mkubwa zaidi, yanaweza kugharimu England katika hatua za mtoano.

MTIHANI HALISI

England imekamilisha kazi ya kufuzu ikiwa kinara wa kundi ikiwa na pointi saba  lakini mtihani wa kweli utaanza katika hatua ya 32 bora.

Hatua ya makundi imeonyesha kuwa timu hii ina vipaji vikubwa vinavyoongozwa na Bellingham na Kane,l lakini pia imeonyesha wazi kuwa bado ina mapungufu makubwa ya kiulinzi.

Ikiwa Tuchel atafanikiwa kuimarisha safu yake ya ulinzi na kurejesha ubora wa kiungo kwa kumtumia Declan Rice ambaye alikosekana, England inaweza kuwa miongoni mwa timu zitakazowania ubingwa.

Lakini kama itaendelea kutoa nafasi nyingi kwa wapinzani kama ilivyofanya dhidi ya Ghana na Panama, basi ndoto ya kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1966 inaweza kuishia katika hatua za mtoano.